Tuesday, October 8, 2024

OFISI YA RAIS-UTUMISHI, KIMBILIO KWA HUDUMA ZA KIUTUMISHI

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi amewapongeza watumishi wa Ofisi yake kwa kutoa huduma nzuri kwa Watumishi na Wananchi wenye uhitaji wa huduma na kuifanya Ofisi hiyo kuwa kimbilio wakati wote kwa huduma za Kiutumishi.

Kaimu Katibu Mkuu huyo ametoa pongezi hizo Oktoba 8, 2024 wakati alipowasili katika Ofisi hizo zilizopo Mtumba, Dodoma kutekeleza majukumu yake ya kila siku na kukutana na watumishi wake waliokuwa wakitoa huduma katika eneo la mapokezi.

“Hakikisheni mnatoa maelezo sahihi na huduma bora na haraka kwa kila Mtumishi au Mwananchi anayekuja kupata huduma katika Ofisi hii, uharaka na ufanisi wetu, utawapa wateja nafasi ya kuendelea na shughuli nyingine za kujenga uchumi wa nchi” amesema Bw. Daudi.

Vilevile, ameongeza kuwa, Wiki hii ni muhimu sana katika usimamizi wa utoaji huduma kwa umma kwa kuwa inasaidia kuimarisha uhusiano baina ya Ofisi na wateja, lakini zaidi kuwafikia Watumishi na Wananchi kwa njia mbalimbali na kutatua shida zao kwa ufanisi na haraka.

Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI Bw. Mussa Magufuli amebainisha kuwa kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja, Ofisi  itahakikisha inakutana na wateja ili kupata maoni, mapendekezo ya kuboresha huduma na kutatua changamoto mbalimbali za kiutumishi zinazowakabili watumishi na wananchi.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka katika wiki ya kwanza ya Oktoba. Kwa mwaka huu, wiki hii imeanza tarehe 7 na itahitimishwa tarehe 11 Oktoba, 2024.






















No comments:

Post a Comment