Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 25 Oktoba, 2024
Mameneja na Wataalam wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya
Umma Barani Afrika wanatarajia kukutana jijini Arusha nchini Tanzania kujadili
mikakatika mbalimbali itatakayosaidia kujenga rasilimaliwatu yenye tija katika
Bara la Afrika.
Hayo yamesemwa leo tarehe 25.10.2024 na Rais wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma
Afrika (APS-HRMNet) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI
na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika
Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Bw. Daudi amesema katika mkutano huo wajumbe watapata
fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalam kwa lengo la kuwezesha nchi za Bara la
Afrika kupiga hatua za kimaendeleo kwa kutumia mbinu za kisasa.
“Mtandao huu umeanzishwa kwa lengo la
kutafsiri mikakati ya maendeleo ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kujenga
uwezo wa rasilimaliwatu yenye matokeo chanya katika kuhudumia wananchi wetu
Barani Afrika.” Bw. Daudi amesema.
Amesema mtandao huo unaundwa na wanachama kutoka Bara
lote la Afrika ambao wamegawanyika katika Kanda tano ikiwemo Afrika Magharibi
yenye Nchi 17, Afrika Mashariki Nchi 10, Afrika ya Kati Nchi 8, Afrika
Kaskazini Nchi 6 na Nchi za Kusini mwa Afrika 13.
Bw. Daudi amesema Tanzania ni nchi mwanachama wa
APS-HRMNet hivyo imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa 9 wa mwaka
utakaowakutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma, Makatibu Wakuu,
Wanataaluma na Wataalam mbalimbali kutoka Barani Afrika.
Mkutano wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu
katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 4
hadi 7 Novemba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Arusha.
Kaulimbiu ya Mkutano huo ni ‘Uhimilivu wa Utawala
na Ubunifu Kukuza Sekta ya Umma yenye Uelekeo wa Baadae Kupitia Uongozi wa Rasilimaliwatu’.
Rais wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika
Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akizungumza na Waandishi wa
habari (hawapo pichani) kuhusu Mkutano wa Mtandao huo utakaofanyika jijini
Arusha kuanzia tarehe 4 hadi 7 Novemba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa jijini Arusha.
Rais wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika
Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi (kushoto) akisisitiza jambo
wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Mtandao huo
utakaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 4 hadi 7 Novemba, 2024 katika Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa jijini Arusha. Kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini wa ofisi hiyo Bi. Mary Mwakapenda.
No comments:
Post a Comment