Na. James
K. Mwanamyoto-Morogoro
Tarehe
15 Mei, 2022
Wajasiriamali mkoani Morogoro wameishukuru
Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge
Tanzania (MKURABITA) kwa kuwapatia elimu iliyowawezesha kurasimisha biashara
zao ambazo zimeboresha maisha yao.
Wajasiriamali hao wametoa pongezi
hizo kwa MKURABITA mjini Morogoro walipotembelewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa
katika banda la MKURABITA wakati wa Maonesho ya Tano ya Mifuko na Programu za
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyohitimishwa jana.
Kiongozi wa Kikundi cha Umoja
Group, kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za sabuni, shampoo na
mafuta ya kupaka, Bi. Lucy Ngulai amesema kabla ya kupatiwa mafunzo na
MKURABITA walikuwa wakiuza bidhaa wanazozalisha kwa kutembeza mitaani lakini
baada ya kupatiwa elimu ya ujasiriamali wameweza kupata leseni ya biashara na
kurasimisha rasmi biashara yao.
“Elimu hiyo ya ujasiriamali tuliyopewa na MKURABITA imetuwezesha kupata fursa ya kunufaika na mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na manispaa ya Morogoro hivyo tumeweza kukuza mtaji wetu,” Bi. Ngulai ameeleza.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Tungi Youth Initiatives kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za viatu, Bw. Raban Anselmo amesema kikundi chake kimenufaika na MKURABITA kwa kurasimisha biashara yao baada ya kupatiwa mafunzo.
Bw. Anselmo amesema kuwa, licha ya MKURABITA kuwapatia mafunzo inawasaidia pia katika kuwatafutia masoko ya bidhaa wanazozalisha ikiwa ni pamoja na kuwaongezea ufanisi kiutendaji.
Naye, mjasiriamali aliyenufaika na MKURABITA ambaye anafanya uzalishaji wa gundi, Bi. Loyce Ntandu amesema awali alikuwa ni mmachinga ambaye anachukua bidhaa dukani na kwenda kuwauzia wateja wake mitaani lakini baada ya kuwezeshwa na MKURABITA amekuwa na ofisi zake ambazo anazitumia kuwahudumia wateja wake.
Bi. Ntandu ameongeza kuwa, MKURABITA imempatia elimu ya namna ya kutunza mahesabu yake ikiwa ni pamoja na kupanga kazi zake kibiashara, hivyo ameishurukuru MKURABITA kwa kumpatia elimu bora iliyomuwezesha kurasimisha biashara yake.
Akizungumzia utendaji kazi wa MKURABITA, Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Deogratius Ndejembi amewaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala
na Serikali za Mitaa kuwa MKURABITA wanafanya kazi kwa kushirikiana na Mamlaka
za Serikali za Mitaa katika kuwezesha urasimishaji wa biashara za wanyonge.
Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, licha ya kufanya
kazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa, MKURABITA pia inafanya kazi na taasisi za
kifedha ili kuwawezesha wananchi wanaopatiwa Hati za Haki Miliki za Kimila
kupata fursa ya kukopa mikopo kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo, biashara
na ujasiriamali ambazo zitaboresha kipato na maisha yao.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa wako kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Morogoro
yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA, ambapo
wamefanikiwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Huduma cha Manispaa ya Morogoro na
kuwatembelea wajasiriamali walionufaika na MKURABITA katika Maonesho ya Tano ya
Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyoanza tarehe 08 hadi 14
Mei,2022 katika Viwanja vya Jamhuri Morogoro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akizungumza na
wajumbe wa kamati yake na watendaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) wakati wa ziara ya kikazi ya siku
mbili ya kamati hiyo mjini Morogoro iliyolenga
kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
akielezea ushirikiano wa MKURABITA na Mamlaka
za Serikali za Mitaa katika kuwezesha urasimishaji wa biashara za wanyonge kwa
Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, wakati wa ziara ya
kikazi ya siku mbili ya kamati hiyo mjini
Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA.
Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha
Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt. Seraphia Mgembe
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa
Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, wakati wa ziara ya
kikazi ya siku mbili ya kamati hiyo mjini
Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA.
Kiongozi wa Kikundi cha Umoja
Group, kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za sabuni, shampoo na
mafuta ya kupaka, Bi. Lucy Ngulai akimueleza Mjumbe wa Kamati ya USEMI Mhe.
Margaret Sitta (Mb) namna MKURABITA ilivyompatia mafunzo ya ujasiriamali
yaliyowawezesha kurasimisha biashara zao.
Katibu wa Kikundi cha Tungi Youth
Initiatives kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za viatu, Bw.
Raban Anselmo akiushukuru Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge
Tanzania (MKURABITA) kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali yaliyowawezesha
kurasimisha biashara zao.
Mjasiriamali aliyenufaika na mafunzo ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali
na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Bi. Loyce
Ntandu akiushukuru
Mpango kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali yaliyowawezesha kurasimisha
biashara zao.
No comments:
Post a Comment