Tarehe 14 Mei, 2022
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma waliohitimu mafunzo ya uongozi katika
Taasisi ya UONGOZI kuhakikisha wanaitumia vizuri elimu waliyoipata katika kusimamia
rasilimaliwatu na rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Mhe.
Ndejembi ametoa nasaha hizo jijini Dar es Salaam kwa wahitimu wa Astashada na Stashahada
ya Uzamili ya Uongozi wa Taasisi ya UONGOZI, katika Mahafali yaliyofanyika
kwenye Ukumbi wa Mlimani City.
Mhe. Ndejembi amesema,
Serikali inatarajia kuona uongozi wa kimkakati kwa wahitimu hao hususani kwenye
eneo la usimamizi wa rasilimaliwatu na fedha ili taifa liweze kunufaika na
elimu waliyoipata.
Ameongeza kuwa, Serikali
inatarajia kuona maboresho makubwa katika nyanja ya mawasiliano na mahusiano miongoni
mwao na baina yao na wadau wa maendeleo kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo
ya taifa.
“Mmefundishwa uzingatiaji wa
maadili, kuongoza kwa kuzingatia misingi ya utawala bora pamoja na kuelezwa athari
za rushwa katika kutekeleza majukumu yenu, hivyo tunategemea mtakaporudi katika
vituo vyenu vya kazi mtakuwa watumishi bora na waadilifu kiutendaji”, Mhe.
Ndejembi amesisitiza.
Naibu Waziri Ndejembi ameeleza
kuwa, mafunzo ya uongozi waliyopatiwa wahitimu hao ni sehemu ya kuwajengea
uwezo wa kusimamia rasilimali za nchi kikamilifu kwa maendeleo ya taifa.
Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa,
kazi ya kuwajengea uwezo kiutendaji iliyofanywa na Taasisi ya UONGOZI kwa
kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aalto cha Finland inaunga mkono jitihada za
Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza mpango wa maendeleo, hivyo ameipongeza
Taasisi ya UONGOZI na chuo hicho kwa kuwajengea uwezo viongozi hao.
“Ni matumaini yangu kuwa
mafunzo haya mliyoyapata yatawawezesha kukuza na kuimarisha uongozi na utawala
bora wenye kuzingatia haki, na uwajibikaji katika maeneo yenu ya kazi, na
kuongeza kuwa ni vema wakatambua kwamba kiongozi mzuri ni yule anayewajibika na
kutekeleza majukumu yake bila kushurutishwa”, Mhe. Ndejembi amehimiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka
viongozi katika Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Umma na binafsi kutenga
fedha za mafunzo kwa ajili ya kuendeleza viongozi katika Taasisi ya UONGOZI ili
waweze kuongeza weledi na kuwa chachu ya maendeleo katika taifa.
Akizungumza kwa niaba ya
wahitimu, Bi. Rabia Mohammed amesema kwa hakika wamepata elimu na kujifunza
mengi ya kiuongozi na si kwa nadharia tu bali kwa vitendo, hivyo wanaahidi
kuyaishi na kuyatendea kazi kwa ajili ya masilahi mapana ya taifa.
Bi. Rabia ametoa wito kwa
viongozi wote wa umma na taasisi binafsi kuzingatia maadili, nidhamu na
uchapakazi na kwa upande wao wanaahidi kuwa mfano wa kuigwa katika uzingatiaji
wa maadili, nidhamu na uchapakazi.
Jumla ya viongozi 117 kutoka
taasisi za umma na sekta binafsi wamehitimu mafunzo ya uongozi yanayotolewa na
Taasisi ya UONGOZI na kutunikiwa vyeti kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada
ya Uzamili ya uongozi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wahitimu wa Astashada na Stashahada ya Uzamili ya Uongozi
wakati wa mahafali ya tano ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Wahitimu
wa Astashada na Stashahada ya Uzamili ya Uongozi wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi alipokuwa akizungumza nao wakati wa mahafali ya tano ya Taasisi ya
UONGOZI yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said akitoa
akihimiza uwajibikaji kwa Wahitimu wa Astashada na Stashahada ya Uzamili ya Uongozi
wakati wa mahafali ya tano ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu Kiongozi Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya UONGOZI, Balozi
Ombeni Sefue akitoa nasaha kwa Wahitimu wa Astashada na Stashahada ya Uzamili
ya Uongozi wakati wa mahafali ya tano ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika
kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
kuzungumza na Wahitimu wa Astashada na Stashahada ya Uzamili ya Uongozi wakati
wa mahafali ya tano ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Aalto cha Finland, Dkt. Pekka Mattila akiwahimiza Wahitimu wa
Astashada na Stashahada ya Uzamili ya Uongozi
kutumia ujuzi walioupata katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wa mahafali
ya tano ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City
jijini Dar es Salaam.
Mhitimu
wa Stashahada ya Uzamili ya uongozi, Bi. Rabia Mohammed akitoa neno la shukrani
kwa niaba ya Wahitimu wa Astashada na Stashahada ya Uzamili ya Uongozi wakati
wa mahafali ya tano ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akimtunuku cheti cha Stashahada ya Uzamili ya Uongozi Mkuu wa Wilaya
ya Temeke Mhe. Jokate Mwegelo wakati wa mahafali ya tano ya Taasisi ya UONGOZI
yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya Wahitimu wakionyesha vyeti walivyotunukiwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
wakati wa mahafali ya tano ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment