Monday, May 16, 2022

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA KIDINI KUTOA HUDUMA ZA KIJAMII NA KULETA MAENDELEO

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 16 Mei, 2022

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeahidi kuendelea kushirikiana na Kanisa la Moravian Tanzania na taasisi zote za kidini nchini katika kutoa huduma bora za kijamii kwa Watanzania zikiwemo za elimu na afya, pamoja na kuleta maendeleo endelevu kwa taifa.

Ahadi hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akimuwakilisha Mhe. Rais katika Ibada ya kumuweka Wakfu Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki.

Mhe. Jenista amesema, Mhe. Rais amemtuma kueleza azma ya Serikali yake kuendelea kushirikiana na Kanisa la Moravian pamoja na taasisi zote za kidini katika kuboresha huduma muhimu za kijamii na kuchangia maendeleo ya wananchi.

Waziri Jenista amewaeleza waumini wa Kanisa la Moravian kuwa, Mhe. Rais amesema atahakikisha yeye na viongozi wote wanaomsaidia kuliongoza taifa wanaendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuheshimu na kuthamini mchango unaotolewa na kanisa katika kutoa huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo kwa taifa.

“Mhe. Rais amenituma niwaambie kuwa, anafahamu na kuthamini sana kazi zinazofanywa na Kanisa la Moravian katika sekta ya afya, anatambua zipo zahanati na hospitali ambazo zinasimamiwa na kanisa la Moravian Tanzania na katika kutoa huduma zinatoa tiba kwa kila Mtanzania bila kubagua itikadi yake ya kidini”, Mhe. Jesita ameeleza.

Akizungumzia mchango wa Kanisa la Moravian katika sekta ya elimu, Waziri Jenista amesema Mhe. Rais anatambua kanisa limeamua kutoa huduma ya elimu ya sekondari na elimu ya juu kwa vijana wa kitanzania pasipo na ubaguzi wowote wa kidini, hivyo Mhe. Rais analishukuru sana Kanisa la Moravian kwa kutoa huduma hizo.

“Mhe. Rais anajua kwamba zipo sekondari tena nyingi tu na zipo shule za msingi na si Bara tu na mpaka Zanzibar pia, ambazo zimejengwa na uongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, kusema ukweli mnafanya kazi kubwa na mnaupiga mwingi kama Mhe. Rais”, Mhe. Jenista amesisitiza.

Aidha, Mhe. Jenista amesema kuwa Serikali inaamini kupitia jitihada za Kanisa la Moravia za kuwajenga waumini wao kiroho, linasaidia na litaendelea kuisaidia Serikali kuwapata viongozi bora ndani ya Utumishi wa Umma ambao watakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ibada ya kumuweka Wakfu Baba Askofu Mteule Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Tanzania imefanyika jana Makao Makuu ya Jimbo la Mashariki, Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Viongozi wa Dini na washarika katika Ibada ya kumuweka Wakfu Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki iliyofanyika Makao Makuu ya Jimbo la Mashariki, Chamazi jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya washarika wakimsilikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao katika Ibada ya kumuweka Wakfu Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki iliyofanyika Makao Makuu ya Jimbo la Mashariki, Chamazi jijini Dar es Salaam.


Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki akiwekwa Wakfu katika Ibada iliyofanyika Makao Makuu ya Jimbo hilo, Chamazi jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimpongeza Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki mara baada ya kuwekwa Wakfu katika Ibada iliyofanyika Makao Makuu ya Jimbo hilo, Chamazi jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifurahia jambo wakati wa Ibada ya kumuweka Wakfu Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki iliyofanyika Makao Makuu ya Jimbo la Mashariki, Chamazi jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akicheza na wanakwaya wa Tabata Moravian wakati wa Ibada ya kumuweka Wakfu Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki iliyofanyika Makao Makuu ya Jimbo la Mashariki, Chamazi jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Viongozi wa Dini mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jimbo la Mashariki, Chamazi jijini Dar es Salaam katika Ibada ya kumuweka Wakfu Baba Askofu Mteule, Mchungaji Lawi Afwilile Mwankuga wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki.


 

No comments:

Post a Comment