Thursday, May 26, 2022

TPSC IMEPEWA DHAMANA YA KUTOA MAFUNZO YA UTOAJI HUDUMA KWA UMMA KUWANUFAISHA WATANZANIA - Mhe. Jenista

Na. James K. Mwanamyoto-Mbeya

Tarehe 25 Mei, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kimepewa dhamana ya kutoa mafunzo yenye tija kwa Watumishi wa Umma na wanaotarajiwa kuhusu utoaji wa huduma bora kwa umma katika fani mbalimbali ili kuwanufaisha watanzania wengi walio kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Mhe. Jenista amesema hayo wakati wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo hicho jijini Mbeya.

Waziri Jenista amesema, kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Serikali inatarajia kuwa na wahitimu wenye weledi, ari, morali na bidii ya kulitumikia taifa ili kutoa mchango kwenye Utumishi wa Umma na hasa kwenye maendeleo taifa.

“Wahitimu wa TPSC mara nyingi wanakuwa wameiva kwenye eneo la uadilifu na weledi, hivyo anataraji watakuwa na mchango kwenye maendeleo ya taifa pamoja na kuwa viongozi na vinara wa uadilifu kwa Watumishi wa Umma na jamii inayowazunguka,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Aidha, Mhe. Jenista amesema kuwa, dhamana hiyo ya kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wahitimu ili wawe na tija katika Utumishi wa Umma na maendeleo ya taifa ni lazima itekelezwe kwa vitendo na menejimenti pamoja na watumishi wote wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka amesema bodi yake ina imani kuwa, wahitimu wamepata mafunzo ya kutosha na wako tayari kulitumikia taifa kwa uadilifu, ujuzi na weledi.

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema, haiba ni jambo linalotarajiwa serikalini kutoka kwa wahitimu wa TPSC ambao watabahatika kuajiriwa na Serikali kwani itawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TPSC, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Emmanuel Shindika amesema chuo chake kinasheherekea Mahafali ya 35 yanayojumuisha wahitimu 1895 kutoka katika Kampasi zote 6 za Dar es Salaam, Tabora, Mtwara, Mbeya, Singida na Tanga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewatunuku vyeti wahitimu hao 1895 kwa ngazi ya Astashahada ya Awali, Astashahada na Stashahada katika fani za Menejimenti ya Kumbukumbu, Mafunzo ya Uhazili, Menejimenti ya Rasilimaliwatu, Utawala wa Umma, Ununuzi na Ugavi pamoja na Utawala wa Serikali za Mitaa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wahitimu wakati wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo hicho jijini Mbeya.

Wahitimu wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na wahitimu hao kabla ya kuwatunuku vyeti wakati wa Mahafali ya 35 ya TPSC yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo hicho jijini Mbeya.

 
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Dkt. Florens Turuka akieleza jukumu la bodi yake, wakati wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo hicho jijini Mbeya.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na wahitimu wakati wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo hicho jijini Mbeya.

 
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Emmanuel Shindika akitoa taarifa ya utekelezaji wa chuo chake kwa Mhe. Jenista Mhagama wakati wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo hicho jijini Mbeya.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiongoza maandamano ya kitaaluma ya wahitimu wakati wa Mahafali ya 35 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo hicho jijini Mbeya.

 

No comments:

Post a Comment