Na. James K.
Mwanamyoto-Moshi
Tarehe 11 Mei, 2022
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Jenista Mhagama amewaasa vijana 350 wanaotarajiwa kuajiriwa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuzingatia mafunzo ya awali ya
uchunguzi yanayotolewa kwa vijana hao katika Shule ya Polisi Moshi ili kuokoa
fedha za umma zinazopotea kutokana ubadhirifu.
Waziri
Jenista ametoa nasaha hizo leo mjini Moshi wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa vijana 350 wanaotarajiwa
kuajiriwa na TAKUKURU mara baada ya kufuzu mafunzo hayo.
Mhe. Jenista
amesema, kama vijana hao watazingatia mafunzo na kuajiriwa, wataisaidia
Serikali kuokoa fedha nyingi zinazopotea kwenye mikono ya watu ambao hawana
uzalendo na uchungu wa maendeleo ya watu, vitu na nchi.
“Mtakapofuzu
mafunzo haya na kupata ajira ya kudumu, tunataka mtoe mchango katika kudhibiti
upotevu wa fedha za umma ili maendeleo ya vitu yaakisi maendeleo ya watu na
maendeleo yote hayo yaakisi maendeleo ya taifa kwa ujumla.” Mhe. Jenista
amesisitiza.
Mhe. Jenista
ameongeza kuwa, vijana hao wakipata mafunzo hayo, yatasaidia pia usimamizi wa
miradi mbalimbali ya serikali na kukamilika kwake kwa wakati, hivyo kuleta
manufaa makubwa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, Mhe.
Jenista ameeleza kuwa dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, TAKUKURU na
Viongozi wengine ni kuongeza nguvu kwenye kuzuia rushwa isitokee kwani gharama
ya kuziuia rushwa ni ndogo kuliko gharama ya kupambana na rushwa, kwa mantiki
hiyo, amewataka vijana hao wanaotarajiwa kuajiriwa na TAKUKURU kuhakikisha
wanaunga mkono kwa vitendo dhamira hiyo ya Mhe. Rais na wasaidizi wake.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP Salum
Hamduni amesema, dhamira ya TAKUKURU ni kuona kila mshiriki anatambua kuwa
ajira yake ndani ya TAKUKURU pamoja na mambo mengine inategemea sana uadilifu
na nidhamu yake wakati wote wa mafunzo na baada ya kuajiriwa.
CP Hamduni amewasihi vijana hao
kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ambayo wanapatiwa na maelekezo mengine
yatakayokuwa yanatolewa na menejimenti ya TAKUKURU pamoja na uongozi wa Shule
ya Polisi-Moshi, na kuongeza kuwa hawatamvumilia yeyote atakayekwenda kinyume
na maadili ya kiutendaji.
Vijana hao 350
wanaopata mafunzo kwa ajili ya kuajiriwa na TAKUKURU ni matokeo ya kibali cha
ajira kilichotolewa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora ili kuiwezesha TAKUKURU kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua
mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa vijana 350 wanaotarajiwa kuajiriwa na Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) yanayofanyika katika Shule ya
Polisi Moshi.
Vijana wanaotarajiwa
kuajiriwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati
akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa vijana hao yanayofanyika
katika Shule ya Polisi Moshi.
Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Mhe. Steven Kagaigai akitoa salamu za mkoa wake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kabla
ya Waziri Jenista kufungua mafunzo ya awali ya
uchunguzi kwa vijana wanaotarajiwa kuajiriwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) katika Shule ya Polisi Moshi.
Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) CP Salum Hamduni akielezea umuhimu wa mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa vijana wanaotarajiwa
kuajiriwa na TAKUKURU kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua mafunzo hayo katika Shule ya Polisi Moshi.
Mkuu wa Shule ya Polisi Moshi, SACP Ramadhani Mungi akielezea maendeleo ya mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
kabla ya Mhe. Jenista kufungua mafunzo hayo kwa vijana 350 wanaotarajiwa
kuajiriwa na TAKUKURU.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Maafisa wa
Jeshi la Polisi katika Shule ya Polisi Moshi alipoenda kufungua mafunzo
ya awali ya uchunguzi kwa vijana wanaotarajia
kuajiriwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Alioambatana
nao ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Steven Kagaigai, Mkurugenzi Mkuu
TAKUKURU CP Salum Hamduni na Katibu
Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Willy Machumu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na
Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wakufunzi wa mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa vijana wanaotarajiwa kuajiriwa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) baada ya kufungua mafunzo hayo
yanayofanyika katika Shule ya Polisi Moshi. Anayefuatia kushoto kwake ni
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Steven Kagaigai na anayefuatia kulia kwake ni
Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU CP Salum
Hamduni.
No comments:
Post a Comment