Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 23 Mei, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi ameitaka
Tume ya Utumishi wa Umma kushughulikia kwa wakati rufaa zilizowasilishwa ili
kuwawezesha warufani kupata haki zao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na
Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo
hayo jijini Dodoma leo wakati akizindua rasmi Tume ya Utumishi wa Umma, ambayo
Makamishna wake wameteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni na
kuapishwa tarehe 21 Mei, 2022 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Naibu Waziri Ndejembi amesema
Tume inazo rufaa na malalamiko mengi ambayo yanatakiwa kutolewa maamuzi hivyo
haina budi kuyashughulikia ili kutenda haki na kuondoa sintofahamu kwa warufani
wanaosubiri hatma ya rufaa zao.
“Wengi wenu hapa Makamisha ni
wanasheria na katika sheria mnasema justice delayed is justice denied
hivyo mkayashughulikie hayo mashauri kwa wakati,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Tume ya
Utumishi wa Umma isipofanya uamuzi sahihi na kwa wakati itaongeza malalamiko
katika Utumishi wa Umma na kukwamisha shughuli za maendeleo na huduma muhimu
ambazo zinazotolewa na waliowasilisha mashauri na rufaa zao.
Akizungumzia utatuzi wa
changamoto ya baadhi ya waajiri na warufani kutowasilisha vielelezo vya rufaa
kwa wakati, Mhe. Ndejembi amesema kuwa ofisi yake inafanya marekebisho ya
Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 ambayo yataipa Tume mamlaka ya
kusikiliza na kutoa maamuzi ya rufaa kwa kutumia vielelezo vya upande mmoja
vilivyopo.
“Kuna mashauri mengi Tume ya
Utumishi wa Umma ambayo yanasababisha Tume kulalamikiwa kwa kutotolea maamuzi,
wakati vielelezo vya mashauri hayo havijawasilishwa, hivyo tumeamua kurekebisha
kanuni ili kuipa Tume mamlaka ya kufanya maamuzi ya rufaa kwa kutumia vielelezo
vilivyopo,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Kwa niaba ya Makamishna wa
Tume ya Utumishi wa Umma, Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji (Mst.) Hamisa
Kalombola amesema kuwa anatambua jukumu kubwa linalowakabili ni kuhakikisha
sheria zinazosimia Utumishi wa Umma zinatekelezwa ipasavyo.
“Tunaahidi kuwa tutatekeleza
jukumu hilo la kuhakikisha sheria za Utumishi wa Umma zinasimamiwa ipasavyo kwa
kuzingatia Haki, Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili
kuhakikisha Watumishi wa Umma wanaendelea kutoa huduma bora kwa umma na kujenga
imani ya wananchi kwa Serikali yao ya Awamu ya Sita,” Mhe. Jaji Kalombola
amesisitiza.
Kwa upande wake Katibu wa Tume
ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama amesema Tume ni mamlaka ya kwanza ya
rufaa katika Utumishi wa Umma hivyo ina wajibu wa kuhakikisha masuala ya
nidhamu katika Utumishi wa Umma yanashughulikiwa kwa misingi ya Sheria, Kanuni
na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Aidha Bw. Kirama ameongeza
kuwa, Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma walioteuliwa na Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan hivi karibuni watapewa mafunzo ya siku tatu ili kuwajengea uwezo
kiutendaji.
Tume ya Utumishi wa Umma inalo
jukumu kubwa la kuhakikisha usimamizi na uendeshaji wa rasilimaliwatu katika
Utumishi wa Umma linatekelezwa kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na
Miongozo mbalimbali ya Utumishi wa Umma iliyopo.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Deogratius Ndejembi akizungumza na Makamishna na watumishi wa Tume ya Utumishi wa
Umma (hawapo pichani) wakati akizindua Tume hiyo jijini Dodoma.
Sehemu
ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Deogratius Ndejembi wakati akizindua Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi
akitoa neno la utangulizi kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi kuzindua Tume ya
Utumishi wa Umma jijini Dodoma.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Deogratius Ndejembi akimkabidhi vitendea kazi mmoja wa Makamishna wa Tume ya
Utumishi wa Umma Mhe. Balozi Adadi Rajabu mara baada ya kuzindua Tume hiyo
jijini Dodoma.
Katibu
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akiwatambulisha Makamishna wa
Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo pichani) kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi kabla
ya Naibu Waziri huyo kuizindua Tume hiyo jijini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji (Mst.)
Hamisa Kalombola akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi mara
baada ya Naibu Waziri huyo kuizindua Tume hiyo jijini Dodoma.
Mwenyekiti
Mstaafu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji (Mst.) Steven Bwana akiwashukuru watumishi wa Tume ya Utumishi wa
Umma kwa kumpatia ushirikiano wakati akitekeleza majukumu ya Uenyekiti wa Tume
hiyo.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna
wa Tume ya Utumishi wa Umma mara baada ya kuizindua Tume hiyo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment