Monday, May 9, 2022

MHE. JENISTA AISISITIZA SUMA JKT KUZINGATIA VIWANGO VYA UBORA WAKATI WAKIKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA OFISI YA KARAKANA YA WAKALA YA NDEGE ZA SERIKALI

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 09 Mei, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amemtaka Mkandarasi SUMA JKT kuzingatia viwango vya ubora wakati wakikamilisha ujenzi wa jengo la ofisi ya karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA).

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA).

Mhe. Jenista amesema pamoja na kutaka kuzingatia muda wa kukamilisha ujenzi ulioanishwa kwenye mkataba wa kukabidhini jengo, lazima viwango vya ubora vizingatiwe.

“Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ukiwa ndiye Mshauri Elekezi hakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa kama tulivyokubaliana kwenye mkataba wetu ili tupate jengo lenye ubora litakalokidhi mahitaji,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, kiasi cha ujenzi kilichobakia cha asilimia 25 iwapo kasi ya ujenzi itaendelea kama ilivyo, ni matumaini yake kuwa tarehe 22 Mei, 2022 jengo litakabidhiwa kama Mkandarasi alivyoahidi.

“Leo nimefurahi na nimeamini kuwa Jeshi halishindwi, ninawapongeza kwa kutekeleza maelekezo yangu niliyoyatoa mwezi Machi, 2022 nilipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi, hivyo tunaamini SUMA JKT mtatukabidhi jengo letu tarehe 22 Mei, 2022.” Mhe. Jenista ameongeza.

Mhe. Jenista amesema kukamilika kwa ujenzi wa ofisi za karakana hiyo ni muhimu kwa usalama wa vyombo vya usafiri wa anga kwa Viongozi Wakuu wa nchi, hivyo ni wajibu wa kila aliyeainishwa kwenye mkataba kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

Kwa upande wake, Meneja Mradi SUMA JKT, Kanali Paul Chiwanga amesema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 75 na kazi zote zilizokuwa zikisababisha mradi kutokamilika kwa wakati zimeshafanyiwa kazi, hivyo ameahidi kukabidhi jengo tarehe 22 Mei, 2022.

Naye mwakilishi wa Mshauri Elekezi Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Mhandisi Dkt. Johnson Malisa amemuahidi Waziri Jenista kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha jengo hilo linakabidhiwa tarehe 22 Mei, 2022.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhandisi John Nzulule amesema SUMA JKT wamejitahidi kutekeleza maelekezo aliyoyatoa Mhe. Jenista mwezi Machi, 2022 wakati wa ziara yake, hivyo amewaomba waendelee kufanya kazi kwa juhudi ili waweze kukabidhi jengo tarehe 22 Mei, 2022 kama walivyoahidi.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelekezo kwa Mkandarasi SUMA JKT ya ukamilishwaji wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jijini Dar es Salaam.  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa Mkandarasi SUMA JKT kuhusu ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jijini Dar es Salaam.  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jijini Dar es Salaam.  


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhandisi John Nzulule akimshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kwa kufanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali jijini Dar es Salaam.  


Meneja Mradi SUMA JKT, Kanali Saul Chiwanga, akimuahidi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kukamilisha ujenzi wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali na kulikabidhi tarehe 22 Mei, 2022 wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Jenista ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jijini Dar es Salaam.  


Muonekano wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali linaloendelea kujengwa jijini Dar es Salaam.  




 

No comments:

Post a Comment