Na. James K.
Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 12 Mei, 2022
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Jenista Mhagama amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na
Utamaduni (UNESCO) linatambua kuwa Tanzania kupitia Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa ina hifadhi kubwa ya nyaraka za utawala wa kijerumani ambazo
hazipatikani sehemu nyingine yoyote duniani.
Waziri
Jenista amesema hayo jijini Dar es Salaam alipokitembelea Kituo cha Kumbukumbu
Kanda ya Mashariki na kujionea nyaraka hizo za kijerumani pamoja na taarifa
hiyo ya UNESCO inayoitambua Tanzania kuwa na kumbukumbu za nyaraka muhimu za
utawala wa Kijerumani.
Mhe. Jenista amesema, kitendo
cha UNESCO kugundua kuwa Tanzania ina nyaraka muhimu za utawala wa kijerumani
zisizopatikana sehemu nyingine duniani, ni jambo la kujivunia kama nchi kwani
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imefanikiwa kuhifadhi nyaraka hizo
ambazo zinalipa taifa heshima kubwa duniani ya utunzaji mzuri wa kumbukumbu za
kihistoria.
“Sasa ni wakati muafaka na
fursa adhimu ya kuzitangaza nyaraka hizi muhimu za kijerumani tulizozihifadhi ambazo
zimepewa heshima ya kutambuliwa na UNESCO kama nyaraka muhimu na maalum ambazo
hazipatikani mahali pengine duniani, ili ziweze kuwa kivutio kikubwa cha
watalii nchini”, Mhe. Jenista amesisitiza.
Waziri Jenista ameongeza kuwa,
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutangaza vivutio vya
watalii kupitia Royal Tour, hivyo
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imuunge mkono kwa kutangaza amali hii
ya nyaraka muhimu za utawala wa kijerumani ili kuongeza idadi ya watalii
watakaoliongezea taifa kipato cha fedha za kigeni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi, amesema nyaraka hizo za utawala wa iliyokuwa German East Africa (Tanganyika, Zanzibar, Burundi na Rwanda) ambayo Makao Makuu yake yalikuwa Dar es Salaam-Tanganyika ziliingizwa kwenye rejesta ya UNESCO ya mwaka 1997 ya Kumbukumbu ya Dunia na kutambuliwa rasmi kama sehemu ya Kumbukumbu ya Dunia (Memory of the World).
Aidha, Bw. Msiangi ameongeza
kuwa idara yake ni ya huduma za nyaraka ambazo hazitumiki kwenye matumizi ya
kawaida ya kila siku lakini zimethibitika kuwa na thamani endelevu katika
historia ya taifa kwenye masuala ya kiutawala, kisheria, kiuchumi na kitafiti.
Akizungumzia mchakato wa
upatikanaji wa nyaraka nyingine zinazohifadhiwa, Bw. Msiangi amesema sheria
inaitaka Idara yake kufanya uchambuzi wa nyaraka kwenye Wizara, Idara
zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka na Taasisi nyingine za Umma ili
kuzihifadhi katika eneo salama kwa sababu idara yake ina wataalam na vifaa vya
vya kuifadhia.
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa inatekeleza shughuli zake kwa mujibu wa Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Na. 3 ya mwaka 2002 na mnamo mwaka 2004 Bunge lilitunga Sheria Sheria Na. 18 ya Mwaka 2004 iliyoiongezea idara hiyo jukumu la Kuhifadhi Nyaraka za Waasisi wa Taifa (Mlm. J.K Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiangalia moja
ya kitabu kinachoelezea historia ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiangalia
ramani inayoonyesha mipaka ya Tanzania wakati wa ziara yake ya kikazi ya
kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini
Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo
ya utunzaji wa nyaraka kutoka kwa Ally Litongolele wakati wa ziara yake ya
kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka
za Taifa jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi hao jijini Dar es Salaam.
Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa
wakimsikiliza Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi hao jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi akielezea
majukumu ya ofisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Jenista ya
kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa
jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika kikao kazi na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na
watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa mara baada ya kuwasili katika Idara hiyo jijini Dar es Salaam
kwa lengo la kuhimiza
uwajibikaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika
picha ya pamoja na Watumishi wa Idara ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa mara baada ya kumaliza kikao kazi chake na
watumishi hao kilicholenga kuhimiza uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment