Na. James K.
Mwanamyoto-Geita
Tarehe 17 Desemba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuelekeza
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule kusimamia maelekezo ya Waziri
Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ya kuhakikisha Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Geita wanaoishi Geita mjini kuhamia maeneo ya jirani na vituo vyao vya kazi ili
waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Waziri Mchengerwa ametoa
maelekezo hayo katika Kijiji cha Kakubilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF mkoani Geita.
Mhe. Mchengerwa amesema, Mhe.
Waziri Mkuu alikwishatoa maelekezo ya watumishi wote wanaofanya kazi
Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuishi katika vituo vyao vya kazi lakini bado
kuna watumishi wanaishi Geita mjini jambo ambalo linaathiri utoaji wa huduma
kwa wananchi.
“Pamoja na maelekezo aliyoyatoa Mhe. Waziri
Mkuu, lakini nimepata taarifa kuwa kuna watumishi bado wanaishi Geita mjini na
sio kwenye vituo vyao vya kazi huku wakitumia gharama za Serikali kuwafikisha
kwenye vituo vyao vya kazi kila siku,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Katika kuhakikisha maelekezo
ya Waziri Mkuu yanatekelezwa kikamilifu, Mhe. Mchengerwa ametoa wiki mbili kwa
watumishi wote wa halmashauri hiyo wanaoishi Geita mjini kuhamishia makazi yao
kwenye maeneo wanayofanyia kazi.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa,
anatarajia ndani ya wiki mbili alizozitoa, watumishi wote wanaoishi mjini
watakuwa wamehamia karibu na maeneo wanayotoa huduma kwa wananchi na kwa kuwa
ana vyanzo vingi vya kupata taarifa, hatosita kuchukua hatua kwa watakaokaidi.
Mhe. Mchengerewa amesema yeye
ni mlezi wa Watumishi wa Umma, hivyo amelazimika kwenda Wilayani Geita ili
kuhakikisha maelekezo ya Waziri Mkuu yanatekelezwa kwa manufaa ya wananchi.
Aidha, Waziri Mchengerwa
amekagua zahanati ya Kakubilo iliyojengwa kwa ufadhili wa TASAF na kuwaahidi
wananchi wa Kijiji hicho kuwa ofisi yake itahakikisha inapeleka watumishi watakaotosheleza
kutoa huduma kwa wananchi.
Mhe. Mchengerwa amehitimisha
ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Geita kwa kuhimiza watumishi kuishi
katika maeneo wanayofanyia kazi ili waweze kuwa na tija katika utoaji wa huduma
kwa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na
wananchi waliofuata huduma za afya kwenye zahanati ya Kakubilo, iliyojengwa na
TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF
mkoani Geita.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kakubilo na watumishi
wa zahanati ya Kakubilo Mkoani Geita kabla ya kukagua zahanati ya kakubilo
iliyojengwa na TASAF kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wa kijiji
hicho na maeneo ya jirani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji
wa miradi ya TASAF mkoani Geita.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiwasili katika Kijiji cha Kakubilo Mkoani Geita kukagua
Zahanati iliyojengwa na TASAF kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wa
kijiji hicho na maeneo ya jirani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua
utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.
Baadhi
ya wananchi wa Kijiji cha Kakubilo mkoani Geita wakimsikiliza Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya
kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.
Baadhi
ya watumishi wa Zahanati ya Kakubilo mkoani Geita wakimsikiliza Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya
kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.
No comments:
Post a Comment