Saturday, December 18, 2021

HAKUNA MRADI ULIONZISHWA NA SERIKALI YA AWAMU YA TANO UTAKAOSHINDIKANA KUTEKELEZWA NA SERIKALI YA AWAMU YA SITA


Na. James K. Mwanamyoto-Chato

Tarehe 18 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hakuna mradi ulionzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano utakaoshindikana kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi wilayani Chato, Mhe. Mchengerwa amewaeleza wananchi hao kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukamilisha utekelezaji wa miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake.

Mhe. Mchengerwa amewasisitiza wananchi hao kufikisha ujumbe kwa wananchi wengine katika maeneo mbalimbali juu ya dhamira hiyo, hivyo waunge mkono jitihada za Mhe. Rais kwa manufaa ya taifa.

Amesema pamoja na dhamira yake ya kukamilisha miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yeye binafsi ametenga fedha ya kutosha kuanzisha miradi mingine ya kuwanyanyua kiuchumi wananchi wa kawaida.

“Mhe. Rais Samia ametenga kiasi cha shilingi bilioni 130 za kuwezesha kuwanyanyua kiuchumi wananchi wa mikoa mitano ikiwemo Geita,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewasisitiza wananchi wa Wilaya ya Chato kuibua miradi itakayotatua changamoto za kijamii ili iweze kutekelezwa na Serikali kupitia fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

“Mhe. Rais Samia amesema fedha anazo za kutosha, hivyo ni jukumu lenu Wanachato kuibua miradi itakayoboresha huduma katika sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Geita yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Chato, mkoani Geita.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki shughuli za ujenzi wa karo kwenye Zahanati ya Nyabilezi iliyojengwa kwa ufadhili wa TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Chato, mkoani Geita. Anayeshirikiana naye ni Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani Chato mkoani Geita.


Walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Chato, mkoani Geita.


 

No comments:

Post a Comment