Tarehe 20 Desemba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika uongozi wake hatowasaliti katika kutetea stahiki zao Watumishi wa Umma wanaofanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo kwa taifa lao.
Akizungumza na Viongozi na
Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Mchengerwa amesema atahakikisha anasimamia
haki na stahiki za Watumishi wa Umma nchini kwa lengo la kuwaongezea morali ya
utendaji kazi kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.
Kufuatia uamuzi wake wa
kusimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa
watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuendana
na kasi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan badala ya kufanya kazi kwa mazoea
kwani wasipowajibika hatokuwa tayari kutetea stahiki zao.
“Pale ambapo tutabaini kuna
mtumishi mzembe, mla rushwa na mbadhirifu wa mali za umma sitokuwa tayari
kumtetea lakini nitakuwa tayari kupambana na kumtetea mtumishi yeyote
mwadilifu, mchapakazi na mzalendo kwa taifa lake muda wote asubuhi, mchana,
jioni na usiku,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amewaelekeza
watendaji kufuatilia utendaji kazi wa watumishi walio chini yao mara kwa mara na
kumtaka kila mtumishi kuongeza ubunifu katika eneo lake la kazi ili aweze kutoa
huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na
taasisi za umma nchini.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka
waajiri kutenga bajeti ya mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji
Watumishi wa Umma walio katika maeneo yao ili waweze kuwa na weledi, ubunifu na
kuongeza ufanisi kiutendaji.
Waziri Mchengerwa yuko kwenye
ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Kigoma yenye lengo la kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa umma na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma
mkoani humo.
Sehemu
ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kigoma wakimsikiliza Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara
yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua
utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kigoma.
Mkuu
wa Mkoa wa Kigoma, CP Thobias Andengenye akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Viongozi na Watumishi wa
Umma wa Mkoa wa Kigoma wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF
mkoani Kigoma.
Mkurugenzi
wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi
akifafanua hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Mkoa wa Kigoma wakati wa kikao
kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa na watumishi wa mkoa huo kilicholenga
kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF mkoani Kigoma.
No comments:
Post a Comment