Tarehe 19 Desemba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amekemea
huduma mbaya zinazotolewa kwa wananchi katika hospitali ya Mkoa wa Kagera.
Akizungumza na Viongozi na
Watumishi wa Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji
kwa watumishi wa umma, Mhe. Mchengerwa amesema, amekuwa akipokea malalamiko mengi
ya wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo kuhusu huduma mbaya zinazotolewa
hospitalini hapo.
Kufuatia malalamiko hayo, Mhe.
Mchengerwa amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issesanda Kaniki
kukutana na watumishi wa hospitali hiyo kwa lengo la kuwahimiza waboreshe
utendaji kazi wao.
“Nimepokea malalamiko mengi kupitia ujumbe
mfupi na kupigiwa simu, watendaji wetu hawana lugha nzuri na utendaji kazi wao
hauridhishi na kuna baadhi wanaomba rushwa kwa wananchi ili wawapatie huduma,
hivyo tubadilike, turudi katika maadili ya taaluma ya kitabibu na misingi ya
utoaji wa huduma bora.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Ili kuhakikisha wananchi
wanapata huduma inayostahili katika hospitali hiyo, Mhe. Mchengerwa amemuagiza
Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Kagera kuwa na utaratibu wa kufanya ufuatiliaji
wa mara kwa mara kwa lengo la kubaini changamoto wanazokutana nazo wananchi hao
na kuchukua hatua stahiki.
Mhe. Mchengerwa ameongeza
kuwa, kutokana na huduma mbaya zinazotolewa na hospitali hiyo, inawalazimu baadhi
ya wananchi kusafiri kwenda mkoa mwingine ili kupata huduma, jambo ambalo
halileti taswira nzuri kwa umma na linawaondolea imani wananchi kwa serikali
yao.
Amesema pamoja na kukemea
kitendo hicho, atawasilisha malalamiko hayo kwenye mamlaka husika zinazosimamia
taaluma za kitabibu ili nazo ziweze kufanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia
taratibu zao za kitaaluma.
Mhe. Mchengerwa amehimiza uwajibikaji
kwa Watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi
kupata huduma bora za kiafya zitakazoimarisha afya zao ili waweze kushiriki
katika shughuli za ujenzi wa taifa.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akisisitiza uwajibikaji kwa Viongozi na Watumishi wa Umma wa
Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma.
Sehemu
ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara
yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.
Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issesanda Kaniki akipokea maelekezo kutoka kwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa ya kuboresha utendaji kazi katika Hospitali ya Mkoa wa
Kagera wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa
Umma wa Mkoa wa Kagera.
Mwakilishi
wa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Bw. Ezekia Nsinkala akipokea maelekezo
kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kufanya ufuatiliaji wa vitendo vya
rushwa katika Hopitali ya Mkoa wa Kagera, wakati wa kikao kazi cha Mhe.
Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera.
No comments:
Post a Comment