Na. Veronica Mwafisi-Mkuranga
Tarehe 29 Disemba, 2021
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi amemchangia fedha ya nauli na ya kununulia vifaa vya shule
mlengwa wa TASAF Bi. Siwema Chikawe, ambaye amewezeshwa na mpango wa TASAF kupata
elimu ya Msingi, kidato cha kwanza mpaka cha nne na kwa sasa yupo kidato cha
tano katika Shule ya Sekondari mojawapo iliyopo Mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Ndejembi ametoa mchango huo, wakati akizungumza na wananchi
na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika
Kijiji cha Kiparang’anda Wilayani Mkuranga.
Mhe. Ndejembi amesema, ameshawishika kumchangia
mwanafunzi huyo kutokana na kazi nzuri iliyofanya na mratibu wa TASAF wilayani
hapo na TASAF Makao Makuu kwa kumpatia ruzuku iliyomuwezesha kuendelea na
masomo.
Akihimiza umuhimu wa elimu kwa walengwa wa TASAF, Mhe. Ndejembi
amemtaka mlengwa huyo kutekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha anasoma kwa bidii
ili hapo baadae aweze kuwa msaada wa kuikwamua
familia yake kutoka katika lindi la umaskini.
“Hakikisha unazingatia masomo ili upate ufaulu mzuri
utakaokuwezesha kujiunga na elimu ya juu kwa manufaa yako binafsi, familia yako
na Taifa kwa ujumla”, Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Kwa
upande wake mlengwa huyo wa TASAF Bi. Siwema Chikawe, ameishukuru TASAF kwa
kumuwezesha kupata mahitaji ya Shule kwani wazazi wake hawana uwezo wa
kumsomesha.
Akieleza
sababu ya familia yake kutokuwa na uwezo wa kumsomesha, Bi. Chikawe amesema
baba yake mzazi hana uwezo wa kuona wakati mama yake mzazi hana kazi rasmi ya
kumuingizia kipato cha kumuwezesha kumudu gharana za masomo yake.
Mhe. Ndejembi
amefanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Mkuranga yenye lengo la kukagua
utekelezaji wa Mpango wa TASAF unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
akizungumza na wananchi na walengwa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
(hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa
miradi ya TASAF.
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji
wa miradi ya TASAF.
Mlengwa wa TASAF Bi.
Siwema Chikawe akitoa ushuhuda kwa Naibu Waziri Mhe. Deogratius Ndejembi wa namna TASAF
inavyomuwezesha kupata mahitaji ya Shule, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijibu hoja za
walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mkuranga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi
ya TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akipokea zawadi ya
bidhaa zinazotengenezwa na walengwa wa TASAF Wilayani Mkuranga wakati wa ziara
yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani humo.
No comments:
Post a Comment