Saturday, December 4, 2021

WAZIRI MCHENGERWA ATAKA CHUO CHA UTUMISHI KUSHIRIKISHA WANANCHI NA KUWATUMIA MAFUNDI WA VETA KUJENGA KAMPASI ZAKE

Na. James K. Mwanamyoto-Singida

Tarehe 04 Disemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameutaka uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kuendelea na utaratibu wa kuwashirikisha wananchi na kuanza kuwatumia mafundi mchundo waliohitimu VETA katika ujenzi wa Kampasi za chuo hicho, ili kuunga mkono azma ya Serikali ya kutoa ajira kwa wananchi.

Waziri Mchengerwa ametoa wito huo akiwa mkoani Singida, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya Singida ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.

Mhe. Mchengerwa amesema, TPSC iendelee na utaratibu huo mzuri wa kuwapa ajira wananchi pamoja na mafundi mchundo waliohitimu VETA ambao wanaishi maeneo yanayozunguka miradi, ili wanufaike na uwepo wa miradi hiyo kwa kuongeza kipato kitakachowawezesha kuboresha maisha yao.

“Utaratibu huu wa kuwatumia wananchi na mafundi mchundo wa VETA usitumike hapa tu kwenye ujenzi wa kampasi hii ya Singida, nataka utumike na kwenye ujenzi wa kampasi nyingine za Tanga na Mbeya,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameutaka uongozi wa TPSC kuzingatia ushauri watakaokuwa wanautoa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ili kukamilisha vizuri ujenzi wa Kampasi za chuo hicho. 

“Mmepata wajumbe wazuri wa bodi ya ushauri ambao wana uzoefu wa kutosha, hivyo wataushauri hatua bora za kuchukua ili kufikia malengo ya ujenzi,” Mhe. Mchengerwa ameongeza. 

Akiwasilisha taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Singida, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika, amesema kwa kushirikiana na Watumishi Housing waliamua kutumia nguvu kazi “FORCE ACCOUNT” ili kuokoa fedha na kutoa fursa kwa wananchi kunufaika kwa kupata ajira.

Sanjali na hilo, Dkt. Shindika amesema chuo kimeunda kamati ya ujenzi inayojumuisha wataalam wa ndani na nje kutoka katika Halmashauri ya Singida na mkoa kwa ujumla ambayo imewezesha kufikia asilimia 15 ya ujenzi ambao ulianza rasmi Agosti 15, 2021.

Kuhusu kukamilika kwa mradi, Dkt. Shindika amesema uongozi wa chuo unatumaini kuwa ujenzi wa kampasi hiyo ya Singida utakamilika kwa wakati, na utasaidia kupunguza gharama ya kukodi majengo ya mtu binafsi ambapo kwa mwaka, chuo kilikuwa kikitumia 87,840,000/=. 

Ujenzi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kampasi ya Singida unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2022.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishuhudia mchoro wa jengo la Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida alipoenda kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi hiyo mkoani Singida.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa maelekezo kwa uongozi wa chuo mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida kabla ya kuweka jiwe la msingi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida.


Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kampasi ya Singida kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kampasi hiyo.


Mwonekano wa jiwe la msingi la Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida aliloliweka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.


Maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kampasi ya Singida.

 

No comments:

Post a Comment