Thursday, December 16, 2021

WAZIRI MCHENGERWA AWATAKA VIONGOZI KUTOZUIA LIKIZO ZA WATUMISHI WA UMMA KWANI NI HAKI YAO KISHERIA

Na. James K. Mwanamyoto-Geita

Tarehe 16 Desemba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema likizo ni haki ya mtumishi kisheria, hivyo hakuna haja ya Kiongozi kuzuia haki hiyo isipokuwa kwasababu maalum ambayo mtumishi husika atashirikishwa.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Mkoani Geita.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Kiongozi anapotaka kuzuia likizo ya mtumishi, afuate taratibu ambazo ni pamoja na kuzungumza na Mtumishi husika anayetaka kuchukua likizo aidha, kwa kumlipa gharama za kuzuia likizo hiyo au kumsogezea muda wa kuchukua likizo hiyo.

Mhe. Mchengerwa amewataka Viongozi kuwa na utamaduni wa kusoma nyaraka mbalimbali za kiutumishi ili kujua sheria na taratibu zitakazowasaidia kuwaongoza pale wanapotaka kutoa matamko yanayozuia stahiki za mtumishi.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, ni vizuri kuzungumza na mtumishi kwa kutumia lugha nzuri na akakuelewa kuliko kutumia cheo ulichonacho au lugha kali kwani unaweza ukazuia likizo yake na asifanye kazi inavyotakiwa.

“Sisi Viongozi tujitahidi sana kujenga matumaini kwenye mioyo ya watumishi tunaowaongoza, tuwasikilize na kutatua kero zao, tuwe karibu nao ili wasiwe waoga na hatimaye kupoteza ubunifu walio nao katika utendaji kazi wao,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Katika kusisitiza maelekezo yake, Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, yeye ndiye Waziri anayesimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, hivyo ni lazima ahakikishe haki za watumishi zinapatikana kwani kama atashindwa kufanya hivyo, atakuwa hana sababu ya kuwepo kwenye wadhifa huo.

Mhe. Mchengerwa yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Geita.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watumishi wa Mkoa wa Geita wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Geita alipowasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Fadhili Juma.


Baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Geita wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akifafanua hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Mkoa wa Geita wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa na watumishi wa mkoa huo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.


Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkuu wa Geita, Bi. Neema William, akiwasilisha hoja za kiutumishi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika mkoa huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiandika maoni yaliyowasilishwa na watumishi wa Mkoa wa Geita wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika mkoa huo.


 

No comments:

Post a Comment