Friday, December 3, 2021

WAZIRI MKUU ARIDHISHWA NA UJENZI WA OFISI YA RAIS-UTUMISHI NA KUZINDUA AWAMU YA PILI YA UJENZI WA MAJENGO 24 YA WIZARA ZOTE

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 03 Disemba, 2021 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuzindua rasmi ujenzi wa awamu ya pili wa ofisi kubwa 24 za Wizara zote zinazojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambazo zitawezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Kassim Majaliwa amezindua ujenzi wa ofisi hizo za Serikali ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya miaka 60 tangu taifa lipate uhuru.

Baada ya kukagua ujenzi wa jengo la UTUMISHI, Mhe. Waziri Mkuu amesema ujenzi huo unaendelea vizuri na kwa viwango vinavyostahili, hivyo unatoa matumani kuwa majengo yote yatakayojengwa yatakuwa ni ya viwango na mazuri.

Kutokana na hatua ya ujenzi iliyofikiwa, Mhe. Majaliwa amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha shilingi bilioni 300 ambazo zinatumika kujenga ofisi za wizara zote kwa kiwango kinachoanzia ghorofa tatu na kuendelea. 

Sanjali na hilo, Mhe. Majaliwa amemthibitishia Mhe. Rais kwamba, ameyakagua majengo na kujiridhisha kuwa ujenzi umeanza na ubora umezingatiwa hivyo, anaamini kuwa yatapatikana majengo yanayokidhi thamani ya fedha iliyotumika.

“Mara baada ya ujenzi wa awamu ya pili wa majengo yote ya wizara katika Mji wa Serikali kukamilika, tutamualika Mhe. Rais aje kuzindua rasmi ofisi hizo ambazo zitawawezesha watumishi wote walio kwenye majengo madogo kuhamia na kutoa huduma kwa wananchi,” Mhe. Kassim Majaliwa ameahidi na kusisitiza.

Mhe. Waziri Mkuu ameongeza kuwa, lengo la uzinduzi wa majengo hayo makubwa ya wizara ni kuwa na mji wa Serikali wa kisasa utakaozingatia dhana ya mji wa kijani yaani ‘GREEN CITY’.

“Tunataka mji huu wa Serikali uwe rafiki, unaovutia na ambao tunaweza kuusemea popote na ndio maana ujenzi wa miundo mbinu yote muhimu unaendelea kwa kasi ukiwemo wa miundombinu ya barabara, maji, umeme ikiwa ni pamoja na kutengwa kwa nafasi za taasisi za kifedha kwenye jengo la uwekezaji la Jiji la Dodoma ili huduma za kibenki zote zipatikane katika mji huo wa Serikali,” Mhe. Majaliwa amefafanua.

Majengo hayo 24 ya Wizara zote za Serikali yanayojengwa katika Mji wa Serikali yatakuwa na uwezo wa kuchukua watumishi wote wa wizara, hivyo, hakutakuwa na mtumishi yoyote wa wizara atakayebakia jijini Dar es Salaam isipokuwa baadhi ya watumishi wa taasisi nyeti ambazo kutokana na asili ya majukumu yake wanalazimika kubakia huko.



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akizungumza mara baada ya kufungua jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za wizara zote baada ya kukagua na kuridhishwa na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akizungumza na wananchi na watumishi wa umma (hawapo pichani) wakati akizindua awamu ya pili ya u jenzi wa ofisi za wizara katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.

 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akiwasili eneo ambalo Ofisi ya Rais-UTUMISHI inajengwa kwa lengo la kukagua na kufungua jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za wizara zote katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.

Ujenzi wa Jengo kubwa la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ukiendelea katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) akifurahia jambo na wasaidizi wake Mhe. Deogratius Ndejembi (wa kwanza kulia), Dkt. Laurean Ndumbaro (wa pili kutoka kushoto) na Dkt. Francis Michael (wa kwanza kushoto) wakiwa katika eneo ambalo Ofisi ya Rais-UTUMISHI inajengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) akifurahia jambo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro, kabla Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) kuwasili katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ili kuzindua awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi za Wizara katika mji huo.







 





 

No comments:

Post a Comment