Na. Mwandishi wetu – Dodoma
Tarehe 17 Juni, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete
(Mb), amesema Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa muhimu
linalowawezesha wananchi kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali
pamoja na namna ya kuzipata kwa urahisi.
Mh. Ridhiwani ameyasema hayo Juni
17, 2026 wakati akifungua maadhimisho ya Wiki ya Utumishi ya Umma yanayofanyika
katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Amesema, maadhimisho hayo yanatoa
fursa kwa Taasisi za umma kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuonesha
mafanikio, ubunifu na maboresho yaliyofanyika katika utoaji wa huduma kwa umma.
Mhe. Ridhiwani amesema
Serikali imeendelea kuimarisha Utumishi wa Umma kupitia maandalizi ya Programu
ya Maboresho ya Utumishi wa Umma yenye lengo la kuongeza tija na ufanisi katika
utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa programu
hiyo itajikita katika maeneo matano ya kimkakati ambayo ni mabadiliko ya fikra
katika Sekta ya umma, ujumuishaji na ushirikishwaji wa Wananchi, uongozi na uwajibikaji,
usimamizi wa Rasilimaliwatu pamoja na mageuzi ya huduma za kidijiti.
Vilevile Waziri Kikwete
amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya
mifumo mbalimbali ya kidijiti ikiwemo e-Utendaji, e-Watumishi, e-Mrejesho,
e-Ardhi, e-Office, TAUSI, GePG, MUVU na MAJIIS ili kuongeza uwazi, uwajibikaji
na ufanisi katika utoaji wa huduma za Serikali.
Akizungumzia Ustawi wa Watumishi
wa umma, Mhe. Ridhiwani amesema Serikali imepandisha vyeo watumishi 219,000
waliokidhi vigezo katika mwaka wa fedha 2025/26 ikiwa ni sehemu ya kutambua
mchango wao na kuongeza motisha kazini. Amesisitiza kuwa zoezi hilo liendelee
kutekelezwa kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo ya Utumishi wa Umma ili
kuhakikisha haki, usawa na uwazi vinazingatiwa kwa watumishi wote.
Katika eneo la ajira, Mhe.
Kikwete amesema Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
imeajiri watumishi 42,500 wa kada mbalimbali katika mwaka wa fedha 2025/26.
Aidha, amesema Serikali imetenga nafasi mpya 45,000 za ajira kwa mwaka wa fedha
2026/27 ili kuongeza nguvu kazi katika sekta mbalimbali za utoaji huduma.
Mhe. Kikwete amesema Serikali
itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na Ustawi wa Watumishi wa Umma kupitia
miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba kwa watumishi wanaofanya kazi katika
mazingira magumu. Amesema Serikali tayari imekamilisha nyumba 54 kwa watumishi
wa sekta za afya na elimu katika mikoa mbalimbali na inaendelea na ujenzi wa
nyumba nyingine 78.
Kwa upande wake Katibu Mkuu-UTUMISHI
Bw. Juma Mkomi amesema ushiriki wa Taasisi nyingi katika maonesho hayo
unaashiria wingi wa Huduma zinazoendelea kutolewa na kuwasihi Wananchi
kutembelea mabanda ya maonesho ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo kupata
ufafanuzi wa masuala ya Kiutumishi na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA pamoja na
huduma zingine kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI kama gazeti la Serikali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiungumza
na Viongozi, Watumishi kutoka Wizara na Taasisi za Umma, pamoja na Wananchi
wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika
katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiungumza
na Viongozi, Watumishi kutoka Wizara na Taasisi za Umma, pamoja na Wananchi
wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika
katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma

.jpeg)

.jpeg)





.jpeg)



No comments:
Post a Comment