Monday, June 8, 2026

NAIBU KATIBU MKUU UTUMISHI AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUWA MABALOZI WA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

 Na Antonia Mbwambo-Dodoma

Tarehe 8 Juni, 2026

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kuzingatia maadili ya kazi, kuwa na tabia njema na kuwahudumia wananchi kwa weledi ili kuongeza ufanisi wa huduma za umma utakaochangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Bw. Daudi ametoa rai hiyo wakati akihitimisha mada ya mafunzo kuhusu Usimamizi wa Utendaji Kazi yaliyotolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi hao Juni 8, 2026   katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.

Bw. Daudi alisema, mafanikio ya Taasisi za Umma hayapimwi tu kwa utekelezaji wa Mipango na Sera, bali pia kwa namna Watumishi wanavyowahudumia Wananchi wanaowategemea katika kupata huduma. Alisisitiza kuwa tabia njema, uadilifu na uwajibikaji ni sifa muhimu zinazopaswa kuonekana kwa kila Mtumishi wa Umma.

“Tunapaswa kutambua kuwa kila Mwananchi anayefika kupata huduma ni mteja muhimu wa Serikali. Jukumu letu ni kuhakikisha anahudumiwa kwa heshima, usikivu na kwa wakati. Hii ndiyo njia bora ya kujenga imani ya Wananchi kwa Taasisi za Umma na kuimarisha utawala bora,” Bw. Daudi alisema.

Aliongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuwa na taifa lenye maendeleo jumuishi, uchumi imara na huduma bora za kijamii, hali ambayo inahitaji Watumishi wa Umma kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa kuzingatia maadili na kuongeza ufanisi katika kazi zao.

Kwa upande wake mwezeshaji kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Oswin Mkinga, alieleza kuwa usimamizi wa utendaji kazi ni muhimu katika kuboresha matokeo ya Taasisi za Umma kwa kuwa utendaji bora huanza kwa upangaji mzuri wa malengo, ufuatiliaji wa utekelezaji wake na tathmini ya mara kwa mara ili kubaini mafanikio na maeneo yanayohitaji maboresho.

Bw. Mkinga alisisitiza kuwa, usimamizi wa utendaji kazi ni chombo muhimu katika kuimarisha uwajibikaji wa Watumishi na kuongeza thamani ya huduma zinazotolewa kwa Wananchi hivyo, ni lazima kila mtumishi akaelewa mchango wake katika kufanikisha malengo ya taasisi na taifa kwa ujumla.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akihitimisha mada ya mafunzo kuhusu Usimamizi wa Utendaji Kazi leo Juni 8, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.



Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika eneo la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.

Afisa kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Oswin Mkinga akifafanua mada kuhusu Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa watumishi wa Ofisi hiyo wakati wa mafunzo ambayo hufanyika kila jumatatu ya wiki katika eneo maalumu la Ofisi hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi hao.


Baadhi ya Wakurugenzi wasaidizi na watumishi kutoka Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika eneo la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.


Baadhi ya  Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika eneo la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment