Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ametoa rai kwa waamini wa Kanisa la Mennonite Tanzania ya kuendelea kulinda umoja, amani, uhuru, mshikamano na ustawi wa watanzania kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania.
Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo wakati
alipomwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye
harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Mkamba cha Kanisa la Mennonite
Tanzania, iliyofanyika katika
kanisa la Mennonite Dayosisi ya Mashariki, Jijini
Dar es salaam.
“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatambua
umuhimu wa elimu kwa watanzania, hivyo anachangia milioni 50 ikiwa ni jitihada
za kuhakikisha kituo kinajengwa haraka ili watoto wetu waweze kupata elimu ya dunia
na ya kiroho, na mimi nilitamani kuchangia milioni 2.5 lakini kwa mahubiri ya
Baba Askofu Gabriel Magwega, Askofu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Dayosisi
ya Mashariki yamenigusa kutoa zaidi, sasa nitatoa sadaka milioni 5 ili kujenga
kituo hiki cha kuandaa rasilimaliwatu” Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene aliongeza kuwa rasilimawatu
ikiandaliwa vizuri na kupata elimu bora, nchi itapata viongozi wenye hofu ya
Mungu na watakuwa na uwezo wa kuongoza nchi kwa kuzingatia maadili mema, hivyo kuleta
maendeleo ya haraka kwa taifa na wananchi kwa jumla.
Aidha, aliongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan iko tayari kushirikiana na Kanisa katika kuondoa maadui
watatu yaani ujinga, maradhi na umaskini. Kwa hiyo ujenzi wa Kituo hicho cha
Elimu cha Mkamba ni msingi wa kupambana na maadui hao.
Awali, Baba Askofu Nelson Kisare,
Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania alisema kuwa Serikali imeridhia Malengo 17 ya Umoja wa
Mataifa kuhusu Elimu (SDG) ambapo katika malengo hayo lengo namba 4 linahusu elimu
hususani Elimu Jumuishi, kwa mantiki hiyo Kanisa la Mennonite Tanzania linaunga
mkono Serikali katika jitihada za kutekeleza malengo hayo kwa kuandaa mazingira
bora ya kutoa elimu kwa watanzania.
Vilevile, aliongeza kuwa Kanisa litaendelea kushirikiana
na Serikali katika utoaji wa elimu bora kwa wasichana na wavulana ili kuunga
mkono jitihada za kuondoa ujinga, maradhi na umaskini. Pia, kanisa litahakikisha
katika shule hiyo linatoa vijana wa kitanzania waliolelewa katika misingi ya
neno la Mungu, wenye kumcha Mungu na wenye hofu ya Mungu ndani ya mioyo yao.
“Waziri, Mhe. Simbachawene tunaomba utufikishie salaam
zetu za shukurani kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupokea barua
yetu, kukubali mwaliko na kukutuma wewe kuja kumuwakilisha, jambo hili ni kubwa
sana na sisi tutaendelea kumuombea kwa Mungu ili aendelee kuongoza nchi hii kwa
amani, furaha na upendo daima” alisema Baba Askofu Kisare.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene akitoa hotuba kwa niaba ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Mkamba cha Kanisa
la Mennonite Tanzania, Jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene akiteta jambo na Baba Askofu Nelson Kisare, Askofu Mkuu wa
Kanisa la Mennonite Tanzania wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo
cha Elimu Mkamba cha Kanisa la Mennonite Tanzania, Jijini Dar es salaam.
Wachungaji
na Waamini wa Kanisa la Mennonite wakifuatilia hatuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George
Simbachawene akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye harambee
ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Mkamba cha Kanisa la Mennonite Tanzania,
Jijini Dar es salaam.
Waumini wa Kanisa
la Mennonite Tanzania, Dayosisi ya Mashariki wakifuatilia hatuba ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye
harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Elimu Mkamba cha Kanisa la Mennonite
Tanzania, Jijini Dar es salaam.