Serikali
imedhamiria kuja na mpango mkakati wa kuongeza bajeti itakayosaidia katika
suala la kuhifadhi na kutunza kumbukumbu na nyaraka za viongozi mbalimbali wa
serikali kwa njia ya tovuti.
Hayo
yamesema na Waziri wa Nchi Ofisi Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya
Hifadhi ya Nyaraka za Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim iliyofanyika katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Simbachawene
amesema kuongezwa kwa bajeti ya kuhifadhi nyaraka kwa njia ya kidijitali
itasaidia vijana na Watanzania kwa ujumla kuweza kusoma na kujua historia ya
nchi yao na Bara la Afrika kupitia viongozi wao.
Aidha
ameeleza kuwa Serikali iko vizuri katika eneo la kuhifadhi nyaraka na tayari
ofisi ya Kumbukumbu na Nyaraka ilishajengwa jijini Dodoma kwa ajili ya kuweka
nyaraka hizo kwa njia ya machapisho na kidijitali.
Mhe.
Simbachawene amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua
mchango wa Viongozi Wastaafu waliolitumikia taifa kwa muda mrefu na kuweza
kutoa maelekezo ya kushirikiana na familia ya Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim kukusanya
nyaraka na kufanikisha uzinduzi wa tovuti hiyo.
“Mhe.
Rais, tunashukuru kwa maelekezo yako uliyoyatoa kupitia Katibu Mkuu Kiongozi
ambaye aliyasimamia kikamilfu na kuweza kufanikisha, hili ni tukio la
kihistoria na linatupa funzo kuwa jambo hili linaweza kufanyika kwa Viongozi
Wastaafu wengine,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Mhe.
Simbachawene amebainisha kuwa ushirikiano wa familia ya Dkt. Salim Ahmed Salim
umekuwa na mchango mkubwa katika kupatikana kwa taarifa za kiongozi huyo ili
ziweze kuhifadhiwa kwenye Tovuti maalum kwa ajili ya kizazi cha sasa na
kijacho.
Ametumia
fursa hiyo kutoa wito kwa viongozi kujenga utaratibu wa kupeleka taarifa zao
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa iliyopo jijini Dodoma ili taarifa zao
ziweze kuhifadhiwa kidigitali kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Waziri wa Nchi Ofisi Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment