Friday, October 27, 2023

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAIDHINISHA VIBALI 930 VYA AJIRA MPYA KWA KADA YA WATUNZA KUMBUKUMBU NA NYARAKA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2023/24

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 27 Oktoba, 2023

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeidhinisha jumla ya nafasi 930 za ajira mpya za kada ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka katika mwaka wa fedha 2023/24 na kutoa nafasi 443 za ajira mpya kwa kada hiyo katika mwaka wa fedha 2022/23.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kufungua Mkutano Mkuu wa 11 wa wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) jijini Dodoma.

Mhe. Simbachawene amesema, uidhinishaji wa vibali hivyo vya ajira mpya unaonyesha ni kwa jinsi gani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kwa ustawi wa taifa.

Ameongeza kuwa, kwa kutambua mchango wa kada hii katika ustawi wa Utumishi wa Umma, jumla ya Watunza Kumbukumbu 649 waliokasimiwa katika Ikama na Bajeti ya mwaka 2022/23 wameshapandishwa vyeo na kuidhinishiwa mishahara ya vyeo vipya mwezi Juni, 2023. 

Katika kushughulikia changamoto za kiutumishi kwa kada hii ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka, Mhe. Simbachawene amesema Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora imekamilisha zoezi la kuhuisha Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada ya Watunza Kumbukubu na Nyaraka na Muundo ambao ulianza kutumika kuanzia tarehe 01 Julai, 2023.

Ili kuongeza ari na morali ya utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma, Mhe. Simbachawene amesema Serikali itaendelea kupandisha vyeo Kada hii na Watumishi wa Umma wengine kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mhe. Simbachawene amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kutoa ushirikiano kwa Viongozi wa TRAMPA na kusimamia utendaji kazi wa Wataalam wa kada hii  pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za kisera na kiutendaji ili kuwezesha utoaji wa huduma bora na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

Mkutano wa wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) hufanyika kila mwaka ambapo wataalam hawa hupata muda wa kujikumbusha masuala mbalimbali yanayohusiana na taaluma yao na mafunzo mbalimbali kuhusu Maadili ya Utendaji kazi, Miundo ya Maendeleo ya Utumishi iliyopo Serikalini ikiwemo kada yao, Uendeshaji wa Serikali, Usalama na Utunzaji Siri za Serikali.  

Mkutano huu wa siku tatu unafanyika kwa kaulimbiu isemayo“Utunzaji bora wa Kumbukumbu na Nyaraka ni Chachu ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa”

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 11 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika jijini Dodoma.




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akitoa maelezo ya awali kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu mkutano wa Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakati wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika jijini Dodoma.


Sehemu ya washiriki wa mkutano wa Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 11 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Dodoma.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Kulia) akipokea zawadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyotolewa na Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) wakati wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Chama hicho uliofanyika jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene aliyekabidhi zawadi hiyo kwa niaba ya chama hicho.





 

 

 

No comments:

Post a Comment