Na. Lusungu Helela-Moshi
07 Oktoba,2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Wahitimu wa Mafunzo ya awali ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwenda kuzuia na kupambana na tatizo la rushwa kwenye miradi mikubwa ya kijamii inayoendelea kutekelezwa sehemu mbalimbali nchini kwani Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mhe. Simbachawene amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora zaidi kwa kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ikiwemo elimu, afya pamoja na maji inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sio kuingia katika mifuko ya watu wachache.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya kufunga Mafunzo ya awali kwa Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi 370 wa TAKUKURU yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Simbachawene amesema, maono na malengo ya Serikali ni kuhakikisha wahitimu hao wanakwenda kuzuia rushwa na ikishindikana kuzuia wakapambane nayo kwani rushwa inapofusha na ni ukosefu wa ustaarabu katika jamii.
“Kazi yenu kuu sio kupambana na rushwa bali kuzuia kabla haijatokea na ndio maana Serikali imeamua kuajiri watumishi wa taaluma mbalimbali wakiwemo Maafisa Ununuzi, Wahasibu, Wasanifu majengo na wataalamu wa TEHAMA ili mkawe mbele katika kuzuia kulingana na taaluma zenu na kushauri ipasavyo mnapoona kuna dalili za rushwa’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene ametoa rai kwa wahitimu hao wa TAKUKURU kutulia katika vituo vya kazi watavyopangiwa na kuachana na mawazo ya kuhamia sehemu nyingine kwa madai ya kutafuta masilahi zaidi.
“Wenye mawazo ya kuwa hapa TAKUKURU mnapita tu naomba niwaambie ukweli, hakuna kitu kama hicho, ninyi mmepewa mafunzo maalum kwa manufaa ya kuwahudumia Watanzania kupitia TAKUKURU na sio kuhamia katika vituo vingine vya kazi,” Mhe. Simbachawene amesisitiza
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amesema ajira hizo kwa wahitimu hao zilikuwa ni za kimkakati lengo likiwa ni kuhakikisha maeneo yaliyokuwa hayawezi kufikiwa na TAKUKURU yanafikiwa kwa sasa na kwa urahisi zaidi.
‘’Mhe. Waziri hawa wahitimu unawaona wengi wao ni Maafisa ambao ni wahitimu katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini katika maeneo tofauti wakiwemo Mainjinia lengo letu ni kuhakikisha mianya yote ya rushwa inadhibitiwa, CP Hamduni ameongeza.’’
Mafunzo haya ambayo ni takwa la kisheria kwa kila mtumishi anayeajiriwa TAKUKURU yamefanyika kwa muda wa miezi mitano kwa Maafisa Uchunguzi na miezi mitatu kwa Wachunguzi Wasaidizi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa TAKUKURU (hawapo pichani) wakati akifunga mafunzo ya awali kwa watumishi hao katika Shule ya Polisi Tanzania, mjini Moshi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja baada ya kufunga mafunzo ya awali kwa Maafisa
Uchunguzi na Wachunguzi
Wasaidizi wa
TAKUKURU katika Shule ya Polisi
Tanzania, mjini Moshi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene akishuhudia gwaride kabla ya kufunga mafunzo ya awali kwa Maafisa
Uchunguzi na Wachunguzi
Wasaidizi wa
TAKUKURU katika Shule ya Polisi
Tanzania, mjini Moshi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene akikagua gwaride kabla ya kufunga mafunzo ya awali kwa Maafisa
Uchunguzi na Wachunguzi
Wasaidizi wa
TAKUKURU katika Shule ya Polisi
Tanzania, mjini Moshi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akitoa zawadi kwa
mmoja wa wahitimu waliofanya vizuri katika mafunzo ya
awali ya Maafisa
Uchunguzi na Wachunguzi
Wasaidizi wa
TAKUKURU katika Shule ya Polisi
Tanzania, mjini Moshi.
Sehemu ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa TAKUKURU wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo ya awali kwa watumishi hao katika Shule ya Polisi Tanzania, mjini Moshi
No comments:
Post a Comment