Na. James K.
Mwanamyoto-Mwanza
Tarehe 3 Mei, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kuzifanyia kazi changamoto za kiutumishi zinazowakabili Watumishi wa Umma kwa muda mrefu ili waweze kutoa huduma bora kwa umma.
Akizungumza wakati wa ziara
yake ya kikazi Mkoani Mwanza leo, Mhe. Mchengerwa amesema hotuba ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Sherehe za Mei
Mosi, 2021 imeainisha wazi azma yake ya kuzifanyia kazi changamoto za Watumishi
wa Umma nchini.
Mhe. Mchengerwa, amesema
hotuba ya Mhe. Rais ni sehemu ya mijadala inayohusu haki na stahili za
Watumishi wa Umma nchini, hivyo hatuna budi kumpongeza kwa kuliona hili na kulitolea
maelekezo, na kuongeza kuwa Watendaji na Maafisa Utumishi watekeleze kikamilifu
maelekezo hayo ili kuondoa changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma.
Ili kuunga mkono azma ya Mhe.
Rais, Mhe. Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kufanya kazi kwa
bidii na uadilifu kwani Serikali ya Awamu ya Sita tangu iingie madarakani ikiwa
ni kipindi cha miezi miwili tu imedhamiria kuondoa kabisa changamoto zinazowakabili
watumishi ili kuwajengea ari kiutendaji.
Akitolea ufafanuzi wa baadhi
ya vipaumbele katika hotuba hiyo, Mhe. Mchengerwa amewasisitiza Watendaji na
Maafisa Utumishi kutoa elimu kwa Watumishi walio chini yao juu ya vipaumbele
hivyo ili Watumishi hao wapate kuelewa kwa ufasaha namna Serikali ilivyowaondolea
changamoto zilizokuwa zikiwakabili.
Akitolea mfano wa kipaumbele
cha punguzo la asilimia moja (1%) ya makato kulingana na stahiki anayopata Mtumishi
wa Umma (PAYE), Mhe. Mchengerwa amesema, Mhe. Rais amewapunguzia mzigo mkubwa
Watumishi wa Umma katika hili na kutolea mfano kuwa mtumishi anayepokea
mshahara wa shilingi laki 3, punguzo la kodi yake ni ni shilingi 30,000 ambayo
ni sawa na kumuongezea Mtumishi wa Umma nyongeza ya mshahara wa shilingi 30,000.
“Natamani sana elimu itolewe
kwa Watumishi juu ya punguzo hili, ili waone ni kwa kiasi gani Mhe. Rais alivyo
na mapenzi mema kwa Watumishi wa Umma.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Pia amewataka Watendaji katika
Taasisi za Umma kutoa ufafanuzi wa vipaumbele vingine vinavyohusu stahiki za
Watumishi wa Umma vilivyoainishwa kwenye hotuba ya Mhe. Rais ikiwemo suala la
punguzo la asilimia 6 ya makato ya Bodi ya Elimu ya Juu na kuongezeka kwa ukomo
wa umri wa watoto kutoka miaka 18-21 kwenye huduma ya Bima ya Afya.
Akizungumzia suala la
upandishwaji wa madaraja, malimbikizo ya madai ya Watumishi, maboresho ya
miundo ya kiutumishi kwa baadhi ya kada na ajira mpya, Mhe. Mchengerwa amesema,
katika kutekeleza vipaumbele vya Mhe. Rais, Serikali imetenga kiasi cha
shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kulipa madai ya watumishi, bilioni 499 kwa
ajili ya upandishwaji wa madaraja, bilioni 120 kwa ajili ya kuboresha miundo ya
baadhi ya kada na zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuajiri Watumishi
40,000 katika sekta ya Afya, Elimu, Ardhi na Kilimo.
Amewasisitiza Watendaji na
Maafisa Utumishi kuzifanyia kazi changamoto za kiutumishi wa watumishi walio
chini yao, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha madai ya watumishi ili yaweze
kuhakikiwa na kulipwa.
Aidha, Mhe Mchengerwa
amesisitiza kushughulikia kwa wakati mashauri ya kinidhamu ya Watumishi wa Umma
ili kuindolea Serikali mzigo wa kulipa fidia pindi Watumishi hao wanapokata
rufaa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na kushinda rufaa zao.
Kuhusiana na mafunzo kwa
Viongozi na Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa amehimiza Waajiri kuhakikisha
wanawapeleka Watumishi kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma na
Viongozi kushiriki mafunzo ya namna bora ya uongozi katika Taasisi ya Uongozi.
Kuhusu mafao ya Wastaafu, Mhe.
Mchengerwa, amewataka Waajiri kuhakikisha wanawasilisha michango ya Watumishi
wa Umma kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati ili wanapostaafu waweze
kupata stahiki zao kwa wakati.
Ziara ya Mhe. Mchengerwa
imelenga kutoa ufafanuzi wa vipaumbele katika hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa
wakati wa Mei Mosi, 2021 na kuhimiza utekelezaji wa vipaumbele hivyo kwa
Watendaji ili kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata stahiki zao mujibu wa
Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watumishi wa Mkoa wa Mwanza leo wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.
Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella.
Baadhi
ya Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
(hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo wakati wa ziara yake ya kikazi
ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.
Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Watumishi wa Mkoa wa Mwanza
leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao.
Mkuu
wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bibi
Hosiana Kusiga akiwasilisha hoja ya kiutumishi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
(hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Waziri huyo ya kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akijibu hoja za kiutumishi za Watumishi wa Umma Mkoa wa
Mwanza leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi
wa Umma mkoani humo. Kushoto kwake ni Naibu Waziri, Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mhe. Angelina Mabula.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akifuatilia taarifa ya utekelezaji ya Mkoa wa Mwanza
aliwapowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo leo ili kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John
Mongella.
No comments:
Post a Comment