Friday, May 28, 2021

UHAMISHO WA WATUMISHI KUFANYIKA KIELEKTRONIKI KUPITIA MFUMO MPYA WA HCMIS KUANZIA MWEZI JULAI, 2021

Na. James K. Mwanamyoto-Sumbawanga

Tarehe 28 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kuanzia Mwezi Julai, 2021 Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara utatumika kuchakata na kuoanisha maombi ya vibali vya uhamisho wa Watumishi wa Umma, hivyo Serikali kwa kiasi kikubwa itapunguza malalamiko ya watumishi kuhusu changamoto iliyopo ya upatikanaji wa vibali vya uhamisho kuchukua muda mrefu.

Dkt. Ndumbaro amesema hayo mjini Sumbawanga wakati akizungumza na watumishi mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma mkoani humo. 

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, mfumo huo utakapoanza kufanya kazi, utaboresha ufanisi wa waajiri katika kuratibu zoezi zima la uhamisho wa Watumishi wa Umma nchini. 

“Baada ya watumishi kuomba uhamisho, maombi yote yataingizwa kwenye mfumo ambapo yatachakatwa, kuoanishwa na kuwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kutoa kibali,” Dkt. Ndumbaro amefafanua. 

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, ili kuhakikisha uhamisho hauibui tatizo la uhaba wa watumishi kwenye maeneo ya uhitaji mkubwa wa rasilimaliwatu, Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakurugenzi Watendaji, Matatibu Tawala Mkoa, Katibu Mkuu TAMISEMI pamoja yeye mwenyewe wamepewa uwezo wa kuona na kuratibu maombi yote ya uhamisho ndani ya maeneo yao ya utawala, hivyo suala la uhamisho litakuwa rahisi kufanyiwa kazi na mamlaka, kwa mantiki hiyo watumishi wataruhusiwa kuhama pasipokuwa na vikwazo visivyo na msingi wowote. 

Kwa upande wake Mtumishi Kilingo ambaye ni Mwalimu, ameipongeza Serikali kwa kuunda mfumo utakaoratibu uhamisho na malipo ya madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi (automatic) na kuongeza kuwa mfumo huo utapunguza kero zilizokuwa zikiwakabili Watumishi wa Umma nchini kwa kipindi kirefu. 

Mwalimu Kilingo amempongeza pia Dkt. Ndumbaro kwa kuupa mkoa wa Rukwa Afisa anayeshughulika na mfumo (approver) anayewajibika kikamilifu tofauti na aliyekuwepo mwanzo ambaye alilalamikiwa kwa kutotekeleza majukumu yake kwa wakati.

Dkt. Laurean Ndumbaro amehitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Rukwa na kuelekea mkoani Katavi kuendelea na ziara yake yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi waliopo katika mkoa huo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao mkoani humo. 


Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao. 


Mwalimu Kilingo wa Manispaa ya Sumbawanga akiipongeza Serikali kuunda mfumo wa kielektroniki utakaoratibu uhamisho na malipo madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa ushauri wa kiutumishi kwa Mwalimu Kiligo wa Manispaa ya Sumbawanga wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Utumishi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Mkoa wa Rukwa. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akifanya mawasiliano kwa njia ya kwa simu ya kiganjani na Afisa wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI aliyepo Dodoma ili kutatua changamoto ya kiutumishi inayomkabili Mtumishi wa Manispaa ya Sumbawanga. 

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitatua changamoto za kiutumishi za watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Utumishi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma mkoani humo. 





 

No comments:

Post a Comment