Tuesday, May 25, 2021

WATUMISHI SONGWE WATAKIWA KUCHAPA KAZI KAMA MHESHIMIWA RAIS ALIVYOELEKEZA ILI KULETA MAENDELEO KWA WANANCHI

Na. James K. Mwanamyoto-Songwe

Tarehe 25 Mei, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewahimiza Watumishi wa Umma wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo kufanya kazi kwa bidii na maarifa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza ili kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaletea maendeleo.

Dkt. Ndumbaro amesema hayo mkoani Songwe akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi mkoani humo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais, ambapo ameambatana na Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ambao kwa pamoja wamehimiza pia ufanisi kiutendaji katika Taasisi zinazosimamia utoaji wa haki kwa wananchi.

Dkt. Ndumbaro amewakumbusha watumishi hao moja ya hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa na kusisitiza Watumishi wa Umma nchini kuchapa kazi tu, na kuongeza kuwa watumishi wakifanya kazi kwa bidii watakuwa wakiunga mkono kaulimbiu ya Mhe. Rais ya Kazi Iendelee ambayo ina manufaa kwa maendeleo ya taifa.

Amefafanua kuwa, Watumishi wa Umma hawana budi kuendeleza utamaduni wa kufanya kazi zenye matokeo chanya, tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amewasisitiza Waajiri na Maafisa Utumishi kutekeleza kwa vitendo azma ya Mhe. Rais ya kuhakikisha Watumishi wa Umma wanapewa haki zao wanazostahili ili kuwajengea morali na ari ya utendaji kazi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome amewataka Watumishi wa Umma nchini kuishi maisha ya kiutumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma ili kufikia malengo ya uwepo wa Utumishi wa Umma.

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewakumbusha watumishi wa Songwe kuwa, muda mwingi wanautumia kazini, hivyo wahakikishe wanaishi vizuri na watumishi wengine mahala pa kazi, na kuongeza kuwa wasipoishi vizuri wataharibikiwa na hatimaye kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya Makatibu Wakuu hao, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Seif Shekalaghe amewaasa watumishi anaowasimamia kubadilika na kuanza kufanya kazi kwa bidii na weledi, na kuongeza kuwa amepokea maelekezo waliyoyatoa na kuahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wake. 

Ziara ya Kikazi mkoani Songwe ya Makatibu Wakuu hao imelenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi mkoani humo, sanjali na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais ya kuhakikisha watumishi wanapata stahili zao kwa wakati ili kuwajengea morali ya kuutumikia umma kwa uadilifu na ufanisi.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na Watumishi wa Umma wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa mkoa huo.

Baadhi ya Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.


Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome akiwasisitiza watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma nchini.


Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiwahimiza watumishi wa Songwe kushirikiana mahali pa kazi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akijibu hoja za Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo walizoziwasilisha wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa mkoa huo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Bi. Hanji Godigodi akiwasilisha changamoto za kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama akiwahudumia watumishi wanaowasilisha changamoto za kiutumishi wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo. 


Afisa Elimu Halmashauri ya Mji Tunduma Bw. Franco Ngonya akiwasilisha changamoto za kiutumishi zinazomkabili kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama akisoma moja ya nyaraka ya mtumishi aliyewasilisha changamoto ya kiutumishi wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Makao Makuu ya Mkoa huo.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe akiwaasa watumishi anaowasimamia kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo waliyoyatoa Makatibu Wakuu wa  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.

 


 

No comments:

Post a Comment