Na. James K.
Mwanamyoto-Zanzibar
Tarehe 11 Mei, 2021
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuboresha maisha ya kaya maskini, urasimishaji ardhi, biashara na utoaji wa fursa za ajira kwa uwiano uliokubalika kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na vikao vya mashirikiano vya Mawaziri kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mhe. Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu ya Zanzibar
alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora ulioongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Ofisi
hiyo, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Mhe. Rais Mwinyi amesema ni
matarajio yake kuona ushirikiano huo ukiendelezwa na kuondoa changamoto za
kiutendaji zilizopo ili wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar wanufaike na masuala
yote yanayohusu MKURABITA, fursa za ajira na ruzuku inayotolewa na TASAF.
Kuhusiana na fursa za ajira
kwa Wazanzibari, Rais Mwinyi amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa utashi wake katika
kusisitiza uzingatiaji wa makubaliano ya uwiano wa Ajira kwa taasisi za Muungano ambapo katika
vikao vya Bunge ilikubalika kuwa Tanzania Bara iwe na asilimia 79% na Tanzania
Zanzibar asilimia 21% ya nafasi za Ajira kila zinapotangazwa.
Akizungumzia suala la kujengeana uwezo kwenye mchakato
wa ajira, Mhe. Rais amesema ni muhimu Zanzibar ikajifunza kutoka Bara kwa kuwa
na kanzidata ya waombaji wa ajira ili fursa za ajira zinapotolewa iwe rahisi
kuwapata watu sahihi wanaohitajika.
Akizungumiza melekezo ya Mhe. Rais Mwinyi, Mhe.
Mchengerwa amesema, Ofisi yake imejipanga kuhakikisha suala la kubadilishana
uzoefu kwa Watumishi wa Umma wa pande zote mbili litafanyiwa kazi.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, atashirikiana na
Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Utumishi wa Umma Zanzibar kuhakikisha Watumishi
wa Umma wanapata mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji ili waweze kutoa huduma
bora kwa wananchi.
“Tutajipanga vizuri kuhakikisha wataalam wa vyuo vya
Utumishi wa Umma Tanzania Bara na Zanzibar wanakutana na kupanga namna bora ya
kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata mafunzo yenye tija katika utumishi wao.”
Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw.
Ladislaus Mwamanga amemueleza Rais Mwinyi kuwa, Serikali imetenga kiasi cha
shilingi bilioni 112.87 kwa upande wa Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu.
Amefafanua kuwa, kiasi hicho kitatumika katika
kutekeleza miradi ya kutoa ajira za muda, ikiwa ni pamoja na kuondoa mapungufu
yaliyopo katika sekta ya elimu, afya na maji na kuongeza kuwa wazee wataendelea
kupata ruzuku kama kawaida kwani hawana uwezo wa kushiriki katika miradi ya
kutoa ajira za muda.
Naye Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe
amesema urasimishaji wa biashara kwa upande wa Zanzibar umefanyika katika
maeneo 8 ambapo wameweza kuwafikia wananchi kwa kutoa mafunzo na kusajili
biashara zao ambapo watu 2926 wamepata leseni za biashara na utambulisho wa
mlipa kodi ambao umewawezesha kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi.
Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw.
Xavier Daudi amesema Ofisi yake iliyoko Zanzibar itahakikisha inatoa elimu kwa
wahitimu ili waweze kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kuomba ajira zinazotangazwa.
Ameongeza kuwa, Ofisi yake hivi sasa imeanzisha
dirisha litakalowawezesha waombaji wa fursa za ajira kupata taarifa za ajira,
kuwasilisha maombi popote walipo na kupata mrejesho wa maombi yao.
Rais Mwinyi amekutana na
ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliolenga
kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania
(MKURABITA) na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa upande wa
Zanzibar.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza
na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
leo katika Ikulu ya Zanzibar wakati ujumbe huo ulioongozwa na Mhe. Mchengerwa
ulipoenda kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa baadhi ya
majukumu ya taasisi zake.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akitoa neno la utangulizi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati Waziri Mchengerwa
alipoenda kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya
baadhi ya majukumu ya taasisi zake.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe.
Haroun Ali Suleiman na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said wakimsikiliza Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi
wakati akizungumza na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora leo Ikulu ya Zanzibar.
Katibu
wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji
wa taasisi yake kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.
Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Ikulu ya Zanzibar.
Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt. Seraphia Mgembe akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa taasisi yake kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Ikulu ya Zanzibar.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi
akitoa maelekezo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Omar Mchengerwa leo katika Ikulu ya Zanzibar
wakati Waziri Mchengewa pamoja na ujumbe wake walipoenda kujitambulisha na
kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa baadhi ya majukumu ya taasisi zake.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi
akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Wa kwanza kulia kwake ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Omar Mchengerwa na wa kwanza kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman
No comments:
Post a Comment