Tuesday, May 4, 2021


Na. James K. Mwanamyoto-Magu

Tarehe 4 Mei, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini nchini kuwa waadilifu katika kuziandikisha kaya zinazokidhi vigezo vya kunufaika na ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.

Mhe. Mchengerwa ametoa onyo hilo kwa Watendaji hao akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa mpango waTASAF wilayani Magu mkoani Mwanza.

Mhe. Mchengerwa amewahimiza Watendaji hao kuongeza umakini katika utambuzi ili zipatikane kaya maskini zinazostahili kupata ruzuku.

“Ikibainika kuna kaya zisizostahili kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskni, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya waliohusika.” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Serikali imedhamiria kuzifikia kaya zote maskini nchini ili kuziwezesha kaya hizo kuboresha maisha yao kwani lengo ni kuzikwamua kutoka katika lindi la umasikini.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka wanufaika wa Mpango wa TASAF kutumia ruzuku kwa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kama Serikali ilivyokusudia.

Ili kuwawezesha wanufaika kutumia vema ruzuku wanayoipata, amewataka Maafisa Ugani wote nchini kuwapa ushauri wa kitaalam wanufaika ili waweze kupata mavuno bora yatakayotokana na ufugaji na kilimo cha kisasa.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Mwanza iliyolenga kutatua changamoto za Watumishi wa Umma, kuhimiza uwajibikaji na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wanufaika na wananchi wa Kijiji cha Nyashigwe, Wilayani Magu mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Mwanza. 



Baadhi ya Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Nyashigwe wilayani Magu Mkoani Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Mwanza. 


Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyashigwe, Bi. Devota Losi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ya Kijiji hicho kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Mwanza.

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji cha Nyashigwe wilayani Magu.

  


Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Nyashigwe wilayani Magu, Bibi Marynsiana Tabu akitoa ushuhuda wa mafanikio aliyoyapata kupitia ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (aliyevaa tai) akielekea kushuhudia mafanikio waliyoyapata wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Nyashigwe wilayani Magu, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji hicho. Wa kwanza kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kalli.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akifurahia mafanikio aliyoyapata mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Nyashigwe wilayani Magu, Bw. Fabian Mtilanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji hicho. 


 

No comments:

Post a Comment