Friday, May 21, 2021

MAKATIBU MAHSUSI NCHINI WATAKIWA KUWA NA LUGHA YA STAHA WAKATI WA KUTOA HUDUMA KWA UMMA

Na. James K. Mwanamyoto-Arusha

Tarehe 21 Mei, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Makatibu Mahsusi kutumia lugha yenye staha wakati wa kuwahudumia watumishi na wananchi wanaofuata huduma katika taasisi zao.

Akifungua mkutano wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Phillip Mpango jijini Arusha, Mhe. Mchengerwa amesema, Makatibu Mahsusi ni kioo cha ofisi yoyote ambayo wageni wanaofuata huduma wanapata taswira halisi ya huduma zitolewazo, hivyo wanapaswa kuwa na kauli nzuri na kutoa huduma bora.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa Makatibu Mahsusi katika uendeshaji wa shughuli za kila siku za ofisi, hivyo hawana budi kuendelea kuilinda imani ya Serikali kwa kuwajibika kikamilifu.

Akizungumzia dhamira ya kuboresha Utumishi wa Umma nchini, Mhe. Mchengerwa amesema hakuna haki isiyokuwa na wajibu, hivyo amewataka Makatibu Mahsusi kutofanya kazi kwa mazoea na wale ambao ni kikwazo katika kutoa huduma wabadilike ili kuendana na azma ya Serikali.

Mhe. Mchengerwa amewaasa Makatibu Mahsusi kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia uadilifu hususan utunzaji wa siri za ofisi na kuongeza kuwa watakaobainika kutozingatia hayo wataondolewa katika ofisi zao.

“Tunahitaji watumishi wachapakazi na waadilifu, kwani dhamira ya serikali ni kusonga mbele, kama utashindwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu utaondolewa bila kujali taasisi uliyopo.” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Katika kuhimiza uadilifu kwa Makatibu Mahsusi, Mhe. Mchengerwa aliwataka Makatibu Mahsusi hao kula kiapo cha Uadilifu kwa Watumishi wa Umma ambapo watumishi hao walitekeleza.

Akifafanua changamoto iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TAPSEA, Bi. Zuhura Maganga kuhusu Makatibu Mahsusi ambao wana umri mkubwa kutothaminiwa hivi sasa na kufikia hatua ya kutopewa kipaumbele kuwahudumia viongozi, Mhe. Mchengerwa amewataka waajiri kuthamini umuhimu wa Makatibu Mahsusi hao ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi kwa kutumia uzoefu walio nao ikiwa ni pamoja na uadilifu na uchapakazi wao.

Ili kuendana na Kaulimbiu ya mwaka huu inayohimiza ubunifu, umahiri na uzingatiaji wa weledi katika utendaji kazi kwa Makatibu Mahsusi, Mhe. Mchengerwa amewataka kuitekeleza kwa vitendo kwa kujiendeleza kitaaluma hususan katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewapongeza viongozi wa TAPSEA kwa kuandaa mkutano huo na kuweka utaratibu wa Makatibu Mahsusi kuchangia damu itakayohifadhiwa katika benki ya damu kwa lengo la kuwahudumia wenye mahitaji katika hospitali mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella amezungumzia umuhimu wa Makatibu Mahsusi na kusema kuwa, watumishi hawa ni muhimu sana kiutendaji kiasi kwamba wakiondolewa hata kwa siku moja, utekelezaji wa majukumu ya taasisi yoyote ile utayumba.

Akitoa nasaha zake kabla ya kumkaribisha Mhe. Waziri kuzungumza na Makatibu Mahsusi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kada ya Uhazili ni kada muhimu sana ambayo inategemewa na viongozi na watumishi wengine katika utendaji kazi wa kila siku, hivyo amewataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja na kutunza siri za ofisi ili kusukuma gurudumu la maendeleo mbele.

Dkt. Ndumbaro amewapongeza Viongozi wa TAPSEA kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo uliohudhuriwa na washiriki wengi ambao watapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kazi, hivyo amewasisitiza kuhamasisha ushiriki wa Makatibu Mahsusi wengi zaidi katika mkutano ujao.

Awali akitoa maelezo kuhusu TAPSEA, Mwenyekiti wa TAPSEA, Bi. Zuhura Maganga alisema Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) kilianzishwa mwaka 2008 kwa lengo la kukuza na kudumisha taaluma ya Makatibu Mahsusi na kuhimiza uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa umma.

Mkutano wa mwaka huu wa TAPSEA unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuwa Mbunifu Mahiri, Zingatia Weledi katika Kuleta Mabadiliko ya Uchumi Tanzania.” ambapo zaidi ya Makatibu Mahsusi 3000 wameshiriki Mkutano huo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Makatibu Mahsusi Jijini Arusha alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA).

 



Baadhi ya Makatibu Mahsusi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akitoa salamu za mkoa wake wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro, akifafanua masuala ya kiutumishi kwa upande wa Tanzania wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) jijini Arusha leo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Seif Mwinyi, akizungumzia masuala ya kiutumishi kwa upande wa Zanzibar wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) jijini Arusha leo.


Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) Bi. Zuhura Maganga akitoa maelezo ya awali kuhusu chama chake wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa chama hicho jijini Arusha leo.

 


Makatibu Mahsusi wakila kiapo cha uadilifu kwa Watumishi wa Umma wakati wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akimkabidhi cheti Mkurugenzi Msaidizi, Bw. Gubas Vyagusa kwa niaba ya Ofisi ya Rais Utumishi cha kutambua mchango wa Ofisi hiyo katika kufanikisha mkutano wa Makatibu Mahsusi wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na mchangiaji wa damu salama alipowasili kufungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Serikali na baadhi ya Makatibu Mahsusi baada ya kufungua mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) leo jijini Arusha.

 


 

No comments:

Post a Comment