Na. James K. Mwanamyoto-Kalambo
Tarehe 27 Mei, 2021
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean
Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na
maeneo mengine nchini kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya
kutoa huduma nzuri kwa wananchi na watumishi wenzao ili wanufaike na huduma
bora zitolewazo na Serikali yao kupitia Taasisi zake.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo akiwa kwenye ziara ya kikazi Wilayani Kalambo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Dkt. Ndumbaro amewaasa watumishi hao kuwajibika kikamilifu kwa kutoa huduma bora pindi wananchi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi kwani wameajiriwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumzia changamoto ya utoaji wa huduma kwa baadhi ya watumishi wa makao makuu ya Halmashauri za Wilaya au Taasisi za Umma, Dkt. Ndumbaro amewahimiza watumishi wote waliopo makao makuu kutoa kipaumbele cha utoaji huduma kwa wananchi na watumishi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu ili kufuata huduma.
Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, kipaumbele cha huduma kikitolewa kwa wananchi na watumishi wanaosafiri umbali mrefu kufuata huduma, hawataingia gharama za malazi kwani watakuwa wamehudumiwa kwa wakati na kurejea katika makazi yao.
“Tumieni saa za kazi ipasavyo kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na watumishi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma badala ya kutumia muda mwingi kwenye mambo yasiyo na tija kwa taifa, Dkt. Ndumbaro amesisitiza.”
Ameongeza kuwa, Watumishi wanaposafiri umbali mrefu kufuata huduma na wasipopatiwa huduma stahiki kwa wakati, watumishi hao wanakosa morali ya kufanya kazi na hatimaye kushindwa kutoa huduma nzuri kwa wananchi hivyo kuibua malalamiko dhidi ya Serikali.
Akitoa shukrani kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Mkuu wa TAKUKURU (W) Bi. Lupakisyo Mwakyolile amempongeza Dkt. Ndumbaro kwa kuitembelea wilaya hiyo iliyopo pembezoni, na kumshukuru kwa kusikiliza na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa wilaya hiyo kwa muda mrefu.
Bi. Mwakyolile amesema, ziara ya Dkt. Ndumbaro imejenga morali ya kufanya kazi kwa watumishi wa Wilaya ya Kalambo na kumhakikishia Dkt. Ndumbaro kuwa watachapa kazi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anavyosisitiza kupitia kaulimbiu yake isemayo KAZI IENDELEE.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
ameanza ziara ya kikazi mkoani Rukwa kwa kuitembelea Halmashauri ya Wilaya ya
Kalambo iliyopo pembezoni ili kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi waliopo katika wilaya hiyo ambapo anatarajia
kuhitimisha ziara hiyo kesho kwa kuzungumza na Watumishi wa Sekretarieti ya
Mkoa wa Rukwa na baadae kuelekea mkoani Katavi kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi waliopo katika mkoa huo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean
Ndumbaro akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo wakati
wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na
kutatua changamoto za watumishi hao.
Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo
wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.
Laurean Ndumbaro wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo yenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Bw.
Palela Msongela akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya wilaya yake kwa Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamoto za kiutumishi.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akijibu hoja za
kiutumishi zilizowasilishwa wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Laurean Ndumbaro
ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi wa Halmashauri Wilaya
ya Kalambo.
Mwalimu Shinuna Khalfan wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo Wilayani humo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za kiutumishi.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akipitia changamoto na kero zilizowasilishwa kwake
na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ili azitatue.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akijibu hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo
yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za kiutumishi.
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kalambo, Bi. Lupakisyo
Mwakyolile akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kalambo, mara baada ya Dkt. Ndumbaro kusikiliza na kutatua kero
zinazowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment