Na. James K.
Mwanamyoto-Zanzibar
Tarehe 12 Mei, 2021
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya mtumishi yeyote atakayesababisha matumizi mabaya ya fedha za ruzuku zinazotolewa kwa kaya maskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.
Mhe. Makamu wa Pili wa Rais ameyasema hayo leo ofisini
kwake alipotembelewa na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora ulioongozwa na Waziri mwenye dhamana ya ofisi
hiyo, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Mhe. Abdulla amesema Serikali
itahakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuzinusuru kaya maskini Zanzibar,
zinatumika kwa malengo yalikusudiwa ili kuboresha maisha ya kaya hizo.
“Ni lazima tuwe na nidhamu ya
kutumia vema rasilimali za umma ikiwemo fedha zinazotolewa na Serikali kwa
ajili ya kuziwezesha kaya maskini.” Mhe. Abdulla amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa amesema ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais Zanzibar inayoratibu masuala ya TASAF itahakikisha inasimamia vema
matumizi mazuri ya fedha za ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya
kuzinusuru kaya maskini.
Aidha, Mhe. Mchengerwa
amewataka Waratibu wote wa TASAF wa Tanzania Bara na Zanzibar kushirikiana
katika kutoa elimu kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili
kuwawezesha kutumia ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao.
Akiwa katika ukaguzi wa utekelezaji
wa miradi ya TASAF ya Kituo cha Afya cha Kianga na shule ya Sekondari ya
Fujoni, Mhe. Mchengerwa amewataka watumishi wa kituo hicho cha afya na wananchi
wanaofuata huduma kukitunza kituo hicho ili kiendelee kutoa huduma bora na kuondoa
adha ya upatikanaji wa huduma za afya ambazo zilikuwa zikiwakabili kabla ya
ujenzi wa kituo hicho.
Akizungumzia ujenzi wa jengo
la shule ya Sekondari Fujoni, Mhe. Mchengerwa amesema, jengo hilo litatatua
changamoto ya kutokuwepo kwa chumba cha kufanyia mitihani kwa wanafunzi wa
shule hiyo ambayo kwa muda mrefu walikuwa wakifanyia mitihani yao chini ya miti
na kupata adha kubwa kipindi cha mvua.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa
TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga aliwashukuru wananchi wa Fujoni kwa jitihada zao
katika kukamilisha ujenzi wa chumba cha kufanyia mitihani.
Bw. Mwamanga amemueleza Mhe.
Waziri kuwa mradi huo umetekelezwa kwa kasi kubwa sana katika kipindi
kisichozidi miezi sita tofauti na maeneo mengine ambayo hutumia mwaka mmoja na
kuongeza kuwa utekelezaji huo unatokana na ushiriki mzuri wa wananchi ambao
walikuwa na hamu kubwa kuhakikisha wanafunzi wanapata eneo zuri la kufanyia
mitihani.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akitoa neno la utangulizi kwa Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati Waziri Mchengerwa alipoenda kujitambulisha na kuwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya baadhi ya majukumu ya taasisi zake.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa
katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora. Wa kwanza kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Omar
Mchengerwa na wa kwanza kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais Zanzibar, Bw. Faina Idarus.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa Fujoni wakati wa ziara yake ya
kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TASAF, Zanzibar.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akipokea taarifa ya utekelezaji ya Kituo cha Afya cha Kianga
kutoka kwa Mkuu wa Kituo hicho, Dkt. Asma Rashid alipokuwa akikagua
utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TASAF, Zanzibar.
No comments:
Post a Comment