Na. James K.
Mwanamyoto-Magu
Tarehe 4 Mei, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi na Watumishi katika Taasisi za Umma kufanya kazi kwa bidii na uadilifu badala ya kuendekeza majungu mahala pa kazi jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya Utumishi wa Umma na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo
leo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa
Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani Magu.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza
kuwa, Watumishi na Viongozi wasiowajibika hawana nasafi katika utawala wa Serikali
ya Awamu ya Sita ambayo imedhamiria kutoa huduma bora kwa wananchi, na kuongeza
kuwa atahakikisha Utumishi wa Umma unakuwa na rasilimaliwatu yenye tija.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa,
Utumishi wa Umma ndio injini ya nchi hii, hivyo Viongozi na Watumishi wa Umma
hawana budi kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuweza kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Mhe. Mchengerwa amesema kuna
baadhi ya Viongozi na Watumishi wenye nyadhifa wamekuwa wakitumia nyadhifa zao
kukandamiza watumishi walio chini yao kwa kusikiliza majungu na fitina.
“Tuache kutumia nyadhifa
tulizo nazo vibaya hivyo tufanye kazi, na kama kuna mtumishi ambaye amekuwa
akitekeleza majukumu yake kikamilifu apewe ushirikiano na andelezwe ili aweze
kutoa mchango mkubwa kwa taifa badala ya kujengewa uadui.
Aidha, amewataka Watumishi wa
Umma kuwa na utamaduni wa kujiendeleza ili waweze kufika mbali. “Jambo lolote
lenye mafanikio ni lazima lianzie mbali, hivyo ni vema kujiendeleza badala ya
kubweteka,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Mhe. Mchengerwa amehitimisha
ziara yake ya kuzungumza na Watumishi Wilayani Magu kabla ya kukagua
utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Kijiji cha
Nyashigwe Wilayani Magu.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu
Mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John
Mongella na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali.
Baadhi ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri
ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
(hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo wakati wa ziara yake ya kikazi
ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na
Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu alipowasili Wilayani hapo kabla ya
kuzungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya leo ili kuhimiza uwajibikaji
kwa Watumishi wa Umma. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John
Mongella na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kali.
No comments:
Post a Comment