Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 28 Januari, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amekemea
tabia ya Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi Serikalini kukwepa jukumu lao la kuwapa
ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi watumishi wanaowasimamia na badala yake huwashauri
kuandika barua kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili
kupewa ufafanuzi wa masuala yao ya kiutumishi.
Mhe. Jenista amesema, barua nyingi za
kuomba ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi zinazowasilishwa ofisini kwake
zinatoka kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri wakati Serikali imeajiri Maafisa
Sheria na Maafisa Utumishi katika Halmashauri zote nchini ili kufanya kazi
hiyo.
“Badala ya nyie Maafisa Sheria na
Maafisa Utumishi kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa watumishi
mnaowasimamia, mnawahamasisha waandike barua kwenye ofisi yangu kupata
ufafunuzi, jambo ambalo si sahihi na halikubaliki,” Mhe. Jenista amefafanua.
Ameongeza kuwa, Maafisa Sheria na
Maafisa Utumishi Serikalini wanatakiwa kutumia nyadhifa zao kuwashauri Viongozi
wao kuwahudumia watumishi ipasavyo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo
inayosimamia Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na maelekezo yanayotolewa na
Serikali.
Mhe. Jenista amehoji uwepo wa Maafisa
Sheria na Maafisa Utumishi katika nafasi zao ikiwa wanashindwa kutatua
changamoto za kiutumishi zinazowakabili watumishi wanaowasimamia ambazo ziko
ndani ya uwezo wao.
“Afisa Sheria au Afisa Utumishi wa
Halmashauri unajisikiaje watumishi katika kituo chako cha kazi kusafiri umbali
mrefu kwa lengo la kuwasilisha masuala yao kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI ili yaweze
kufanyiwa kazi wakati na wewe upo na masuala hayo yapo ndani ya uwezo wako
kiutendaji,” Mhe. Jenista amehoji.
Mhe. Jenista amesema kuwa, kuna barua
nyingine ukisoma na kufanya uchambuzi unabaini kuwa mtumishi ameonewa na
mwajiri wake na mwajiri huyo huyo anamshauri mtumishi huyo kuwasilisha suala
lake Ofisi ya Rais Utumishi badala ya kulitatua.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Mhe. Waziri kufungua kikao kazi hicho, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema, ofisi yake
imeandaa kikao kazi hicho kwa lengo la kutatua changamoto ya baadhi ya Maafisa
Sheria na Maafisa Utumishi kutozingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo
katika utendaji kazi wao.
Bw. Daudi amesema Maafisa Sheria na
Maafisa Utumishi wana jukumu kubwa la kuhakikisha Sheria, Kanuni, Taratibu na
Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo inafuatwa ili kutenda haki katika utoaji
wa huduma bora kwa umma.
Kikao kazi hicho cha siku mbili kimeandaliwa
na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na
kinahudhuriwa na Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi wa Halmashauri za Wilaya 35
nchini.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akifungua kikao kazi cha Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria
kutoka Halmashauri za Wilaya 35 za Tanzania (hawapo pichani) jijini Dodoma.
Sehemu ya Maafisa
Utumishi na Maafisa Sheria wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo
pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi cha watumishi hao jijini Dodoma
kilicholenga kutatua changamoto katika utekelezaji wa sheria ya Utumishi wa
Umma na Kanuni zake.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi cha Maafisa Utumishi na
Maafisa Sheria jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa kikao kazi
cha Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria, Bw. Maganiko Msabi akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama mara baada ya Mhe. Jenista kufungua kikao kazi cha Maafisa hao
jijini Dodoma.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria
mara baada ya kufungua kikao kazi cha watumishi hao jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment