Saturday, January 29, 2022

TIMU YA WATAALAM YAUNDWA KUAINISHA MAPUNGUFU YA OPRAS NA KUPENDEKEZA MFUMO MPYA UTAKAOONGEZA UWAJIBIKAJI-Mhe. Jenista

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 29 Januari, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, ofisi yake imeunda kikosi kazi maalum cha wataalam wabobezi kinachoendelea kufanya mapitio na kuainisha mapungufu yote ambayo yamejitokeza kwenye Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa watumishi (OPRAS) ili kupendekeza mfumo mpya wa kielektroniki wa wazi na rafiki ambao utaondoa upendeleo, udanganyifu na kuongeza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.

Akizungumza na Watumishi wa Umma kupitia vyombo vya habari jijini Dodoma, Mhe. Jenista amesema, ofisi yake imechukua hatua hiyo ya haraka kuunda kikao kazi hicho ili kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye azma yake ni kuwa na mfumo bora wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma tofauti na mfumo wa OPRAS uliopo hivi sasa, ambao umebainika kuwa na mapungufu ambayo hayatoi matokeo halisi ya utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja.

“Katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais, Ofisi yangu imeamua kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kuunda timu hii maalum ya wataalam wabobezi ili kuhakikisha tunapata mfumo bora, imara na wenye tija ambao utaondoa changamoto za utekelezaji zilizojitokeza katika mfumo wa OPRAS unaotumika hivi sasa, uliosanifiwa mwaka 2004,” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, timu hiyo ya wataalam imemthibitishia kuwa, mfumo huo mpya wa kielektroniki wa upimaji wa utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja unaopendekezwa utakuwa ni mfumo rafiki na wenye manufaa kwa Watumishi wa Umma, ambao utarahisisha uandaaji wa mikataba ya utendaji kazi na kutoa fursa ya kujiwekea malengo na shabaha kwa kila mtumishi.

“Mfumo huo mpya utapunguza muda wa Watumishi wa Umma kucheza na makaratasi na utawataka viongozi wenye dhamana ya usimamizi wa watumishi kutimiza wajibu wao kwa kufanya ufuatiliaji, kupima na kutoa mrejesho wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma bila kuwaonea, kuwakandamiza ama kutumia hila ya aina yoyote,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imejipanga kuhakikisha mfumo huo mpya wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma uanze kutumika rasmi tarehe 01 Julai, 2022.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Umma kupitia vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu uboreshaji wa masuala mbalimbali ya kiutumishi.


Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao kupitia vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu uboreshaji wa masuala mbalimbali ya kiutumishi.


 

No comments:

Post a Comment