Na.
Veronica Mwafisi-Nkasi
Tarehe 19 Januari, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anawajali wananchi
wanyonge ndio maana ameongeza shilingi Bil. 5.5 kwenye Mpango wa TASAF ili kaya
zote maskini ambazo ni walengwa wa mpango huo zinufaike.
Mhe.
Ndejembi amesema licha ya Mhe. Rais kuelekeza fedha nyingi kwenye shughuli
mbalimbali za kijamii, ameona ni vema kutenga fedha zaidi kwa ajili ya
utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini ambao kwa kiasi kikubwa
unazisaidia kaya maskini kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini.
“Serikali
ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya kila
kitu kuuongezea nguvu ya kiuchumi Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili uweze
kutekeleza vizuri Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini, hivyo ni jukumu la
kila mlengwa kuitumia vizuri ruzuku anayoipata kuboresha maisha yake,” Mhe.
Ndejembi amefafanua.
Ili kuboresha zaidi maisha ya walengwa hao, Mhe. Ndejembi amewataka
walengwa kuona umuhimu wa kuunda vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitawawezesha
kupata sifa kukopeshwa na Halmashauri.
“Ninatamani kuona baada ya kuanzisha vikundi vyenu vya
ujasiriamali muende Halmashauri kuomba mkopo wa asilimia kumi (10%)
utakaowawezesha kufanya shughuli za maendeleo ambazo zitaboresha maisha ya
familia zenu,” Mhe. Ndejembi amehimiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewaeleza wanufaika hao kuwa, kwa zile Kaya
ambazo bado zinasubiri kuingia kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini,
utaratibu unafanyika na muda si mrefu wataingizwa katika Mpango huo.
Kwa upande wake mlengwa wa
TASAF, Bi. Scolastica Tinga wa Kijiji cha Kipundi, amemshukuru sana Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Mlengwa huyo ameishukuru pia
TASAF kwa kumpatia ruzuku iliyomuwezesha kujenga nyumba bora ya kuishi, kwani kabla
ya kuanza kupokea ruzuku toka TASAF hakuwa na nyumba bora ya kuishi.
Naye, mlengwa mwingine wa
TASAF, Bi. Leticia Futakamba wa Kijiji cha Kipundi, amesema Mpango wa TASAF
umemuwezesha kuwasomesha watoto yatima anaoishi nao, kulima shamba
lililomuwezesha kupata chakula cha mwaka mzima ikiwa ni pamoja na kumuwezesha
kufyatua tofali 2800 ambazo atazitumia kujengea nyumba yake iliyobomoka.
Mhe. Ndejembi amefanya ziara
ya kikazi Wilayani Nkasi, yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa
Umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa
na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akizungumza na walengwa wa TASAF Wilayani Nkasi wakati wa ziara yake
ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Walengwa wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Wilaya ya Nkasi wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji
wa miradi ya TASAF.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akizungumza na walengwa wa TASAF (Hawapo pichani) Wilayani Nkasi wakati
wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya
hiyo. Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Mhe. Aide Kenan na
kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijualikali.
Mwakilishi wa
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu (aliyesimama) akitoa ufafanuzi
wa utoaji wa ruzuku kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wakati wa
ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF
katika Wilayani Nkasi.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(katikati) akisikiliza hoja za walengwa wa TASAF Wilayani Nkasi wakati wa ziara
yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika wilaya hiyo.
Mlengwa
wa TASAF Bi. Scolastica Tinga wa Kijiji cha Kipundi, akitoa ushuhuda wa namna
alivyonufaika na TASAF kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wa namna TASAF wakati wa
ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa
miradi ya TASAF.
Bi. Fedelika Kitao wa Kijiji cha Kipundi akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa
kumpatia fedha za kujenga banda la kuhifadhia mifugo lililoharibika kutokana na
mvua.
No comments:
Post a Comment