Thursday, January 20, 2022

MHE. NDEJEMBI AELEKEZA KUFANYIKA KWA UCHUNGUZI WA UJENZI WA OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI SUMBAWANGA

 

Na. Veronica Mwafisi-Sumbawanga

Tarehe 20 Januari, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuelekeza Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Sumbawanga, Bw. James Mbungano kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na mchakato wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sumbawanga katika Mji mdogo wa Laela.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, baada ya kushuhudia msingi wa jengo hilo la ghorofa ukifukuliwa ili kujengwa upya kwa viwango vinavyotakiwa.

Mhe. Ndejembi amesema, kitendo cha msingi wa jengo la ofisi hizo kufukuliwa kwa ajili ya kujengwa upya maana yake ni kuwa, kuna changamoto katika mchakato mzima wa kandarasi hiyo.

“Tumemsikia wenyewe Mhandisi akisema kuwa kulikuwa na changamoto ya mawasiliano kabla ya kuanza kwa ujenzi, hii ina maanisha kwamba kuna tatizo hapa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Ameongeza kuwa, kunapokuwa na makosa ya kimawasiliano ni ishara ya kukosekana utawala bora hivyo, Serikali inachokiangalia ni thamani ya fedha inayotolewa katika ujenzi kama inalingana na kiwango cha ujenzi.

Mhe. Ndejembi amemuhoji Mkandarasi anayesimamia ujenzi huo, Bw. Yohane Renatus kuhusu sababu ya ujenzi wa jengo hilo kutokamilika kwa wakati, na kuelekeza kasi ya ujenzi iongezwe bila kuathiri viwango stahiki.

Amesema haiwezekani fedha ya Serikali ikachezewa halafu Serikali ifumbie macho, hivyo itaendelea kuchukua hatua kwa watakaobainika ili thamani ya fedha iliyotumika ionekane kwa umma.

“Kama kuna watu wa kuwachukulia hatua tutawachukulia, huu ni uzembe, Mhe. Mkuu wa Wilaya tuanze uchunguzi wa mchakato mzima ili kubaini ulivyofanywa katika kumpata Mkandarasi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kwela, Mhe. Deus Sanga amesema tangu wiki iliyopita ameweka kambi katika eneo hilo ambalo ujenzi wa Ofisi hiyo unaendelea ili kuhimiza ufanisi katika ujenzi.

Amesema pamoja na kuweka kambi katika eneo hilo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji, lakini watendaji wa Kampuni ya MUST ambao ndio wajenzi wa Ofisi hizo wamekuwa wakitoa sababu zisizoridhisha kuhusu kutokamilika kwa ujenzi wa jengo hilo.  

Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wapili kutoka kushoto) akitazama maendeleo ya ujenzi wa jengo la ghorofa la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sumbawanga katika Mji mdogo wa Laela wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji katika Wilaya hiyo.

 

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (watatu kutoka kulia) akimuhoji Mkandarasi Bw. Yohane Renatus sababu za kutokukamilika kwa wakati ujenzi wa jengo la ghorofa, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sumbawanga katika Mji mdogo wa Laela wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya hiyo.


 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wakisikiliza taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la ghorofa, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sumbawanga katika Mji mdogo wa Laela wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo katika Wilaya hiyo.


 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wapili kutoka kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Sebastian Waryuba (aliyenyoosha mkono) alipokuwa akieleza kuhusu Kampuni ya MUST inasuasua kukamilisha kwa wakati ujenzi wa jengo la ghorofa, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sumbawanga katika Mji mdogo wa Laela wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya hiyo.

 

 

No comments:

Post a Comment