Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 15 Januari, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka
watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kujipanga kiutendaji
ili kuhakikisha wananchi na Watumishi wa Umma wanaohudumiwa na ofisi yake
wanafurahia huduma zinazotolewa.
Mhe. Jenista ametoa wito huo jijini
Dodoma, wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa
Rasilimaliwatu Serikalini chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa
idara hiyo.
Mhe. Jenista amesema kuwa, anataka
ufike wakati mtumishi wa umma anayedai haki ambayo amedhurumiwa kwa muda mrefu
na mwajiri wake pindi akisikia kuwa suala lake limewasilishwa Ofisi ya
Rais-UTUMISHI afurahi na kuwa na matumaini kuwa litafanyiwa kazi kwa wakati.
“Nataka Mtumishi wa Umma aliyekata
tamaa ya kutolipwa malimbikizo yake ya mishahara au kupewa stahiki zake
nyingine akisikia suala lake limewasilishwa Idara ya Usimamizi wa
Rasilimaliwatu Serikalini afurahi na kuamini kuwa suala lake litafanyiwa kazi
kwa haki na wakati,” Mhe. Jenista amefafanua.
Waziri Jenista ameongeza kuwa, Idara
hiyo ikifanya kazi kwa uadilifu na weledi itakuwa imetoa mchango mkubwa katika
kujenga morali ya utendaji kazi wa Watumishi wa Umma nchini, ikiwa ni pamoja na
kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi na
Watumishi wa Umma kuutumia vema mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (www.swu.go.tz)
kuwasilisha changamoto na malalamiko ya masuala ya kiutumishi na utawala
bora ili yaweze kufanyiwa kazi na hatimae wananchi wanufaike na huduma
zinazotolewa na taasisi za serikali.
“Mimi Waziri mwenye dhamana ya
kumsaidia Mhe. Rais kusimamia masuala ya kiutumishi na utawala bora napenda nipokee
changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma kupitia mfumo huu hivyo, watumishi
muutumie ipasavyo,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista anaendelea na vikao kazi
na Watumishi wa Ofisi yake tangu aapishwe hivi karibuni na Mhe. Rais kuwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu
Serikalini
jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la
kujitambulisha na kutoa mwongozo wa utendaji kazi anaouhitaji. Kushoto
kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier
Daudi.
Sehemu ya Watumishi wa Idara
ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
alipokuwa akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao jijini Dodoma wakati wa kikao
kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo wa
utendaji kazi anaouhitaji.
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa
Rasilimaliwatu, Bi. Jeanfrida Mushumbushi akieleza namna Mfumo Mpya wa
Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara unavyofanya kazi kwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na Watumishi wa Idara ya
Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini alichokifanya jijini Dodoma kwa lengo la
kuhimiza uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment