Saturday, January 22, 2022

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAJENGEWA UWEZO KIUTENDAJI KUENDANA NA KASI YA UTENDAJI KAZI WA MHE. RAIS

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 22 Januari, 2022

Watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wanapatiwa mafunzo yatakayowajengea uwezo na ufanisi kiutendaji ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Kaulimbiu yake ya KAZI IENDELEE ambayo lengo lake kuu ni kuwapatia Watanzania huduma bora.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utawala, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Salome Kessy amesema, ofisi imeandaa mafunzo hayo kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

“Mafunzo haya yatatukumbusha utendaji kazi unaozingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma ili tuweze kufanya kazi kwa bidii na kuendana na kaulimbiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE,” Bi. Salome amefafanua.

Ameongeza kuwa, mafunzo haya yatajenga uadilifu kwa watumishi na kuwa chachu ya kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.

“Ni matarajio ya ofisi kuwa, baada ya watumishi wote kupata mafunzo haya watakuwa na uwezo na ufanisi mkubwa wa kutoa huduma bora kwa umma,” Bi. Salome amesisitiza.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Katibu Mahsusi, Bi. Alfonsina Mkanyia ameishukuru Menejimenti ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kuwa na utendaji kazi unaoendana na Kaulimbiu ya Mhe. Rais ya KAZI IENDELEE.

Bi. Alfonsina amesema kuwa, mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa wa kiutendaji na kuwapatia morali ya kutoa huduma bora kwa wateja wa ndani na nje.

Naye, Msaidizi Mkuu wa Kumbukumbu, Bi. Theresia Riwa ameshukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo katika muda muafaka na kuahidi kuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi kwa uadilifu ili kuiishi kwa vitendo kaulimbiu ya Mhe. Rais ya KAZI IENDELEE.

Mafunzo haya kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yametolewa kwa kundi la kwanza linalowajumuisha Makatibu Mahsusi na Wasaidizi wa Kumbukumbu na yataendelea kutolewa kwa makundi mengine ya watumishi.


 

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia kwa makini mada inayowasilishwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo kiutendaji ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Kaulimbiu yake ya KAZI IENDELEE.


Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utawala, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Salome Kessy akiwahimiza washiriki wa mafunzo kutumia vema elimu waliyoipata katika utendaji kazi wao ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Kaulimbiu yake ya KAZI IENDELEE.

 

 

1 comment:

  1. Do you want to increase your website's domain authority (DA) score without using any black hat SEO technique then please read this link - https://how-to-increase-da-of-website-online.blogspot.com/

    ReplyDelete