Na. Veronica Mwafisi-Songwe
Tarehe 21 Januari, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni wa kimkakati na kipekee kwasababu unamfikia mlengwa moja kwa moja kwenye Kaya yake na kumuwezesha kuboresha maisha yake.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Mkoani Songwe wakati wa kikao kazi chake cha kuhimiza uwajibikaji kwa Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa TASAF.
Mhe. Ndejembi amewasisitiza maafisa hao kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya walengwa wa TASAF ili miradi hiyo iwe na tija katika kuboresha maisha yao.
Ameongeza kuwa, lengo la Serikali kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini ni kuzinyanyua kimaisha Kaya maskini, hivyo amewataka maafisa kuratibu shughuli za TASAF kwa weledi mkubwa ili kuisaidia serikali kufikia lengo lake.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF, Mkoa wa Songwe, Bi. Atusungukye Dzombe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa maelekezo aliyowapatia na kuahidi kuwa atahakikisha wanayafanyia kazi ili kaya lengwa ziondokane na umaskini.
Naye, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mbozi, Bi. Agnes Mwansembo, amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwapa maelekezo yatakayoboresha utendaji kazi katika uratibu wa utekelezaji wa mpango wa TASAF, na kuongeza kuwa katika wilaya yake wamehamasisha uanzishwaji wa vikundi vya ujasiriamali na tayari wamefikia hatua ya utengenezaji wa Katiba ambayo itawawezesha walengwa hao kunufaika pia na mikopo ya Halmashauri.
Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Waratibu wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakati wa Kikao kazi chake na Waratibu hao kilichofanyika Mkoani Songwe.
Baadhi ya Waratibu wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa Kikao kazi chake na Waratibu hao Mkoani Songwe.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji-TASAF, Bw. Oscar Maduhu (aliyesimama) akitoa ufafanuzi wa hoja iliyowasilishwa na mmoja wa Waratibu wa TASAF wakati wa Kikao Kazi cha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kilichofanyika Mkoani Songwe.
Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Bw. George Kibona akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kuwapa maelekezo ya kusimamia utekelezaji wa Mradi wa TASAF wakati wa Kikao Kazi chake na Waratibu wa (TASAF) kilichofanyika Mkoani Songwe.
Do you want to increase your website's domain authority (DA) score without using any black hat SEO technique then please read this link - https://how-to-increase-da-of-website-online.blogspot.com/
ReplyDelete