Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 11 Januari, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema
amedhamiria kuimarisha misingi ya utendaji kazi kwenye Utumishi wa Umma ili
wananchi wanufaike na huduma zitolewazo na taasisi za umma nchini.
Mhe. Jenista ametoa ahadi hiyo leo
jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Idara za Uendelezaji
Sera na Utawala wa Utumishi wa Umma.
Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, ujio
wake katika ofisi hiyo, sio wa kutengua torati, bali ni kuendeleza mazuri
yaliyofanywa na mtangulizi wake na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha
Utumishi wa Umma.
“Ninaposema sijaja kutengua torati
nina maana ya kuwa nimekuja kuongeza nguvu kiutendaji ili kumsaidia Mhe. Rais
kuboresha Utumishi wa Umma na kuendeleza mazuri yaliyokwishafanyika na
watangulizi wangu,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Waziri Jenista ameongeza kuwa,
atatumia dhamana aliyopewa na Mhe. Rais kutatua changamoto zinazowakabili
Watumishi wa Umma ili waweze kuwa na morali ya kutoa huduma bora kwa umma.
“Tunaona imani kubwa aliyo nayo Mhe.
Rais kwa Watumishi wa Umma, hivyo nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya
kumsadia kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora, nitahakikisha Watumishi wa
Umma wanafanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuendana na kauli mbiu yake ya
KAZI IENDELEE.” Mhe. Jenista amefafanua.
Mhe. Jenista amesema Mtumishi wa Umma
ana mchango mkubwa wa kutimiza ndoto ya Mhe. Rais ya kuleta maendeleo kwa wananchi
na ndio maana amekuwa akiwahimiza waajiri kuwapatia Watumishi wa Umma stahiki
zao kwa wakati ili wawe na ari kiutendaji.
Mhe. Jenista ameanza vikao kazi na Watumishi wa Ofisi yake mara baada ya kuapishwa rasmi na Mhe. Rais kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera na
Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma leo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi
chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo wa
utendaji kazi anaouhitaji. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius
Ndejembi.
Sehemu
ya Watumishi wa Idara ya Uendelezaji Sera wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
alipokuwa akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao leo jijini Dodoma wakati wa
kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo
wa utendaji kazi anaouhitaji.
Sehemu
ya Watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama alipokuwa akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao leo jijini Dodoma
wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na
kutoa mwongozo wa utendaji kazi anaouhitaji.
No comments:
Post a Comment