Na. Veronica Mwafisi-Songwe
Tarehe 22 Januari, 2022
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi amewataka waratibu wa TASAF kuhakikisha trilioni 2.2
zilizotolewewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Kuzinusuru Kaya Maskini
zinatumika ipasavyo kuboresha maisha ya wazee, wanawake, walemavu na vijana
walio katika kaya hizo.
Mhe.
Ndejembi amesema, anatamani kuona walengwa wa TASAF wanasimamiwa vizuri ili wawe
na vikundi vya ujasiriliamali ambavyo vitapata mkopo wa asilimia 10 katika
Halmashauri na kutumia mikopo hiyo na ruzuku wanayoipata kunyanyua maisha yao
kiuchumi.
“Walengwa
wa TASAF wakiwemo wazee, wanawake, walemavu na vijana wakiunda vikundi na
kujishughulisha na ujasiriamali watakuwa kwenye mazingira mazuri ya kujikwamua kutoka
katika hali duni waliyonayo,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Aidha, Mhe.
Ndejembi amewataka waratibu wa TASAF kuhakikisha wanashirikiana na wataalam wa Idara
za kilimo, mifugo na maendeleo ya jamii kuwatembelea walengwa wa TASAF mara kwa
mara ili kuwapatia ujuzi na utaalamu utakaowasaidia kuwa na vikundi bora vitakavyowawezesha
kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi
Mtendaji waTASAF Bw. Oscar Maduhu amemshukuru Mhe. Rais Samia Sulluhu Hassan,
kwa kuwapatia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi
huo wa TASAF.
Bw. Maduhu amesema, katika kuhakikisha mradi huo
wa TASAF unatekelezwa vizuri, wamejipanga kuhakikisha wanawawezesha walengwa kuondokana
na lindi la umaskini na kuwa na hali bora ya maisha.
Mhe. Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi katika
mikoa ya Rukwa na Songwe aliyoifanya kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifafanua
jambo kwa wandishi wa habari kuhusu ziara ya kikazi aliyoifanya
katika mikoa ya Rukwa na Songwe iliyokuwa na lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi wa TASAF katika mikoa hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
akisikiliza swali toka kwa mwandishi wa habari kuhusu ziara yake ya kikazi aliyoifanya
katika mikoa ya Rukwa na Songwe iliyokuwa na lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi wa
TASAF katika mikoa hiyo.
Muwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji
wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu (Wakwanza kushoto) akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa TASAF katika mikoa ya Rukwa na Songwe mara
baada ya kukamilika kwa ziara ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ya kukagua
utekelezaji wa miradi wa TASAF katika ya mikoa hiyo.
No comments:
Post a Comment