Tuesday, January 18, 2022

MHE. JENISTA AMUOMBA MUNGU KUMPA HEKIMA NA BUSARA KATIKA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA WATUMISHI

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 18 Januari, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amemuomba Mwenyezi Mungu kumpa hekima na busara kila anaposhughulikia masuala yote ya kiutumishi yanayohusu ustawi wa Watumishi wa Umma na Sekta ya Utumishi wa Umma kwa ujumla ili aweze kumsaidia vema Mhe. Rais kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini.

Mhe. Jenista amesema kuwa, hekima na busara ndio nyenzo pekee itakayomuwezesha kuwatendea haki Watumishi wa Umma pindi anapofanya maamuzi yanayohusu mustakabali wa stahiki za Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kukisimamia vema Chuo cha Utumishi wa Umma ambacho kina jukumu kubwa la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kwenye eneo la uadilifu na utendaji kazi.

“Ninamuomba Mwenyezi Mungu aniongoze mimi na wasaidizi wangu kuwa na hekima na busara zitakazotuwezesha kufanya kazi kwa bidii na uadilifu katika kumsaidia Mhe. Rais kutimiza azma yake ya kuwaletea maendeleo Watanzania,” Mhe. Jenista amefafanua.

Akizungumzia umuhimu wa Chuo cha Utumishi wa umma Tanzania, Mhe. Jenista amesema, chuo kina nafasi kubwa ya kuwajengea uwezo kiutendaji Watumishi wa Umma ili waweze kufanya kazi kwa kuzingatia miiko na maadili ya Utumishi wa Umma.   

Waziri Jenista amesema kuwa, Chuo cha Utumishi wa Umma kwa mujibu wa uzoefu wake katika Utumishi wa Umma, ndio chuo pekee chenye sifa stahiki ya kutoa mafunzo yatakayojenga misingi imara ya Utumishi wa umma nchini.

“Elimu yetu hivi sasa ni huria, mtu yeyote anaweza kwenda kusoma chuo chochote ndani au nje ya nchi lakini atakapoingia kwenye Utumishi wa Umma ni muhimu akapata mafunzo elekezi TPSC ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa umma iliyopo,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Kutokana na umuhimu huo wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Mhe. Jenista ametoa wito kwa waajiri wote katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanatenga bajeti zitakazowawezesha Watumishi wanaowasimamia kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji katika chuo hicho.

Mhe. Jenista ameanza ziara ya kikazi ya kuzitembelea taasisi zilizo chini ya ofisi yake kwa lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma ambapo ameanza kukitembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa hivi karibuni na Mhe. Rais kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa chuo hicho. 


Sehemu ya watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa chuo hicho. 


Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa chuo hicho. 


Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa chuo hicho. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa TPSC. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akishuhudia wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakipiga chapa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa TPSC.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipokea vitendea kazi vya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania toka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka na Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa TPSC. 


 

No comments:

Post a Comment