Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 18 Januari, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza
Menejimenti ya Watumishi Housing kuangalia uwezekano wa kujenga nyumba za
kuwauzia na kuwapangisha Watumishi wa Umma waliopo katika Wilaya na Mikoa yenye
uhitaji badala ya kutoa kipaumbele kikubwa cha ujenzi wa nyumba hizo mijini.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo
mara baada ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za Watumishi wa Umma
zilizojengwa na Watumishi Housing eneo la Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es
Salaam.
Mhe. Jenista amesema kuna uhitaji
mkubwa wa nyumba za watumishi katika Halmashauri za Wilaya na Sekretarieti za
Mikoa hususan kwa Walimu, Watumishi wa Sekta ya Afya, Askari wa Jeshi la Polisi
na Watumishi wa Kada za chini, hivyo ni vema Watumishi Housing ikawa sehemu ya
utatuzi wa changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa, katika kutatua
changamoto hiyo ya upungufu wa nyumba za watumishi, Ofisi yake itashauriana na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuona namna bora ya kuitumia
Watumishi Housing kujenga nyumba za watumishi.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejenga vituo vya afya katika kila Halmashauri
ya Wilaya na kupeleka Watumishi wa kutoa huduma katika vituo hivyo, hivyo
wanahitaji nyumba kwa ajili ya kuishi ili waweze kufanya kazi kwa ufasaha,”
Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista ametoa wito kwa
Watumishi wa Umma kupanga na kuzinunua nyumba zinazojengwa na Watumishi Housing
kwani ni za gharama nafuu kwa asilimia 10 mpaka 30 ya bei za nyumba zilizoko
kwenye soko.
Mhe. Jenista ameishauri Watumishi
Housing kushirikiana na Halmashauri ili kupata viwanja vya gharama nafuu
vitavyowezesha kujenga nyumba ambazo Watumishi wenye kipato cha chini watamudu
kupanga na kuzinunua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji
wa Watumishi Housing, Dkt. Fred Msemwa amemhakikishia Mhe. Jenista kuwa ataisimamia
taasisi yake katika kutekeleza maelekezo aliyoyatoa ili watumishi wanufaike na
nyumba za gharama nafuu.
“Nikuhakikishie Mhe. Waziri, mimi na
wasaidizi wangu tutaendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii ili kukidhi
azma ya Serikali ya kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata nyumba za gharama
nafuu,” Dkt. Msemwa ameahidi.
Mhe. Jenista amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili jijini Dar es Salaam ya kutembelea Chuo cha Utumishi wa Umma na Watumishi Housing kwa lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji katika taasisi hizo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akikagua miradi ya Watumishi Housing eneo la
Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa
taasisi hiyo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akisalimiana na mkazi wa nyumba zilizojengwa na Watumishi
Housing eneo la Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa
taasisi hiyo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Watumishi Housing (hawapo pichani) jijini
Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.
Sehemu ya watumishi
wa Watumishi Housing wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara
ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred
Msemwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya
taasisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe.
Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akitoa maelekezo kwa Menejimenti ya Watumishi
Housing baada ya kukagua mradi wa taasisi hiyo eneo la Gezaulole, Kigamboni
jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi ya
kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.
Mkuu wa
Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa akieleza umuhimu wa mradi wa Watumishi
Housing katika Wilaya yake wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ya
kukagua mradi ya Watumishi Housing eneo la Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es
Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Watumishi Housing Company, Dkt. Fred Msemwa akieleza namna miradi ya
ujenzi wa nyumba inavyotekelezwa na taasisi yake wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama ya kukagua mradi ya Watumishi Housing eneo la Gezaulole,
Kigamboni jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment