Na.
James K. Mwanamyoto – Morogoro
Tarehe 21 Disemba, 2020
Tatizo la Watumishi wa Umma
kukaimu nafasi za uongozi kwa muda mrefu bila kupata stahili ya vyeo wanavyokaimishwa,
linatokana na waajiri kutozingatia taratibu za kiutumishi pindi wanapowakaimisha
watumishi hao kama Waraka wa Utumishi Namba 2 wa Mwaka 2018 unavyoelekeza.
Hayo yamesemwa leo Mkoani
Morogoro na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika alipoitembelea Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa huo kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na
utawala bora.
Mhe. Mkuchika amesema,
kumekuwa na tabia ya Waajiri wengi hususan katika halmashauri kuwakaimisha
watumishi ambao hawana sifa za kukaimu wala kibali cha kukaimu ambacho
kinatolewa na Katibu Mkuu - UTUMISHI.
Mhe. Mkuchika amefafanua
kuwa, ili mtumishi aweze kukaimu, anapaswa kuwa na cheo cha Afisa Mwandamizi na
kuendelea na pia awe amepatiwa kibali cha kukaimu nafasi husika na Katibu Mkuu-
UTUMISHI ambacho atakitumikia kwa miezi isiyozidi 6 kabla ya kithibitishwa
rasmi iwapo atakidhi vigezo vya kukitumikia cheo hicho.
Mhe. Mkuchika ameongeza
kuwa, kitendo cha Watumishi kukaimishwa bila kufuata taratibu kimekuwa ni
chanzo cha malalamiko ya watumishi wengi, hivyo amewataka Waajiri kuzingatia
taratibu ili kuepuka malalamiko ambayo yanashusha morali ya utendaji kazi.
Wakati huo huo, Mhe. Mhe.
Mkuchika amewataka Waajiri kuhakikisha wanawawezesha wastaafu kupata mafao yao kwa
wakati pindi wanapostaafu ili kuwaondolea usumbufu wa wa kufuatilia mafao yao
pindi wanapostaafu ikizingaatiwa kuwa wamelitumikia taifa kwa bidii na
uadilifu.
Mhe. Mkuchika amesema, ili
Wastaafu wapate mafao kwa wakati, Maafisa Utumishi wanapaswa kufanya maandalizi
kwa kukusanya vielelezo vyote vinavyohitajika mapema miezi 6 kabla.
"Kutokana na changamoto
hii, nitafanya mkutano na Maafisa Utumishi nchi nzima kama nilivyoahidi hapo
awali ili kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu suala hili,” Mhe. Mkuchika
amesisitiza
Awali, akiwasilisha taarifa
ya utekekezaji ya Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi
Emmanuel Kalobelo alimwambia Mhe. Waziri kuwa, pamoja na mafanikio mazuri
yaliyopatikana katika Mkoa wa Morogoro, Ofisi yake ina changamoto ya watumishi
kukaimu kwa muda mrefu na wastaafu kutokapata mafao yao kwa wakati pindi
wanapostaafu.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt.
(Mst) Mhe. George Mkuchika akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa
Morogoro (hawapo pichani) alipoitembelea Ofisi hiyo kwa lengo la kupata taarifa
ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.
Baadhi
ya Watendaji wa Mkoa wa Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George
Mkuchika (hayupo pichani) alipoitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa
lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na utawala
bora.
Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Ole Sanare akielezea changamoto za kiutumishi
za Mkoa wake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika, alipoitembelea Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa huyo kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya
kiutumishi na utawala bora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George
Mkuchika akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, alipoitembelea
Ofisi hiyo kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi
na utawala bora.
No comments:
Post a Comment