Wednesday, December 23, 2020

TAASISI YA UONGOZI YATAKIWA KUWAPIKA VIONGOZI WA AINA ZOTE BILA KUJALI TOFAUTI ZAO

Na James Mwanamyoto - Dar es Salaam

Tarehe 23 Desemba

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameitaka Taasisi ya Uongozi kuwaandaa Viongozi wa aina zote bila kujali tofauti zao ili waweze kutoa mchango katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya Uongozi yenye lengo la kufahamiana na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa taasisi hiyo.

Mhe. Ndejembi amesema Taasisi ya Uongozi ikijikita katika kuwaandaa viongozi bora itakuwa ni taasisi ya mfano na kuigwa Barani Afrika jambo ambalo litaleta sifa nzuri kwa nchi yetu.

“Taasisi ya uongozi ikifanikiwa kuwaandaa viongozi bora nchini, itawawezesha Watanzania popote walipo kujivuna kwa kuwa na taasisi yenye mchango mkubwa wa kutoa mafunzo kwa watu waliopewa mamlaka ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo”, Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewahimiza watumishi wa Taasisi ya Uongozi kuwa na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo ili iweze kufikia malengo iliyojiwekea.

Akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo amesema taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kuandaa na kuendesha mafunzo ya viongozi, kuendesha majadiliano ya kisera na kufanya tafiti za kisera, kutoa ushauri wa kitalaam kuzisaidia taasisi na viongozi wake kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Taasisi ya Uongozi ilianzishwa Julai, 2010 lengo likiwa ni kuwa na Kituo cha utalaam wa juu cha kuendeleza Viongozi Barani Afrika kwa kuanzia Tanzania, Kanda za Afrika Mashariki na hatimaye Afrika nzima.




Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Uongozi (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Taasisi hiyo na kuhimiza uwajibikaji. Kulia kwake ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo.


Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Ndejembi aliyoifanya leo katika taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana na watumishi wa Taasisi hiyo na kuhimiza uwajibikaji.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifuatilia historia ya Taasisi ya Uongozi iliyokuwa ikiwasilishwa leo na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Taasisi hiyo na kuhimiza uwajibikaji.


Watumishi wa Taasisi ya Uongozi, wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Ndejembi katika taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Taasisi hiyo na kuhimiza uwajibikaji.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Taasisi ya Uongozi wakati wa ziara yake ya kikazi leo Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Taasisi hiyo na kuhimiza uwajibikaji.


 

No comments:

Post a Comment