Friday, December 18, 2020

CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KUJENGA KAMPASI KANDA YA ZIWA ILI KUTOA MAFUNZO KWA WATUMISHI NA WANANCHI

 

Na. James K. Mwanamyoto – Chato

Tarehe 19 Disemba, 2020

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kiko mbioni kujenga kampasi Wilayani Chato, Mkoani Geita itakayotoa fursa ya mafunzo kwa Watumishi wa Umma na wananchi wa Kanda ya Ziwa.

Akikagua eneo litakalojengwa Kampasi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika ameridhika na eneo lililotengwa kwani ni rafiki kwa usalama na utoaji wa elimu.

Mhe. Mkuchika amesema, Kanda ya Ziwa pekee ndiyo ilikuwa haijabahatika kuwa na Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma, hivyo fursa hii ni muafaka na itakuwa na manufaa kwa Watumishi wa Umma na wakazi wa eneo la Kanda hii.

Akizungumzia uamuzi wa kujenga Kampasi hiyo Wilayani Chato, Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Chato imetoa kiwanja hicho bure tofauti na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa ambayo yangekigharimu Chuo fedha nyingi kununua kiwanja.

Mhe. Mkuchika ameishukuru halmashauri kwa kutoa kiwanja na kumhimiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa hati kwani Chuo kiko tayari kuanza ujenzi mapema iwezekavyo.

Naye Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika amewathibitishia wakazi wa Kanda ya Ziwa kuwa, fedha za kuanza ujenzi zimeshapatikana, hivyo kinachosubirikiwa ni hati.

“Tukikabidhiwa hati ya kiwanja, tutaanza ujenzi wa madarasa mapema iwezekanavyo ili wakazi wa Kanda ya Ziwa wanufaike na huduma zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma kama ilivyo katika Kanda zingine,” Dkt. Shindika amesisitiza.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani amemtaka Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo kuwasilisha maombi ya kupatiwa umeme katika eneo hilo ili kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa kampasi hiyo.

Mhe. Kalemani ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kampasi hiyo ambayo itatoa fursa ya mafunzo na ajira kwa wakaohitimu na kuongeza kuwa, chuo kitajengwa eneo ambalo ni salama na kitalindwa kwa ushirikiano wa wananchi.

Akizungumzia eneo ambalo Chuo kitajengwa, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi amesema, ujenzi wa kampasi hiyo ukikamilika, itakuwa ni chachu ya maendeleo kutokana na muingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali watakaokuja kupata mafunzo na utavutia uwekezaji.

Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato itakayojengwa eneo la Rubambangwe lenye ekari 41.66 itahudumia Mikoa ya Geita, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika akielezea mpango wa kujenga kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Wilayani Chato, Mkoani Geita alipoenda kukagua eneo ambalo Kampasi ya chuo hicho itajengwa. Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani na Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika.



Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika akimuonyesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika mchoro wa Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato inayotarajiwa kujengwa Wilayani humo. Wanaoshuhudia ni Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi.


Sehemu ya kiwanja ambayo kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato itajengwa. Wanaoonekana katika picha ni baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Serikali wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika.


Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika kuhusu mchoro wa Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato utakavyokuwa. Miongoni mwa wanaoshuhudia ni Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi.

Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani akimuahidi Mhe. Mkuchika kuharakisha upatikanaji wa umeme katika eneo ambalo kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato itajengwa.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika na Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani     wakifurahia jambo mara baada ya kupata maelezo ya ujenzi wa kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Wilayani Chato inayotarajiwa kujengwa hivi karibuni.


 

No comments:

Post a Comment