Tuesday, December 22, 2020

WATUMISHI HOUSING YATAKIWA KUTUMIA ‘FORCE ACCOUNT’ KATIKA MIRADI YA UJENZI WA NYUMBA ILI KUWAWEZESHA WATUMISHI KUPANGA NA KUNUNUA NYUMBA





Na James Mwanamyoto - Dar es Salaam

Tarehe 22 Desemba, 2020.

 

Watumishi Housing Company imetakiwa kuacha kuendelea kutumia Wakandarasi katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za kuwauzia na kuwapangisha Watumishi wa Umma na badala yake watumie ‘force account’ ili kuokoa gharama na kujenga nyumba ambazo watumishi wataweza kupanga na kuzinunua.

Maelekezo hayo yametolewa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Watumishi Housing Company ikiwa ni pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake.

Mhe. Ndejembi amesema madhumuni ya kuanzishwa kwa Watumishi Housing Company ni kujenga nyumba za gharama nafuu zinazoweza kununuliwa na Watumishi wa kada zote, hivyo hakuna sababu ya kutumia wakandarasi ambao gharama zao za ujenzi ni kubwa na kusababisha gharama kubwa za upangishaji na uuzaji wa nyumba hizo.

“Watumishi wa Umma wanajitoa sana katika kulitumikia taifa hili, sasa ni wakati wa Serikali kutambua mchango wao kwa kuwawezesha ikiwa ni pamoja na kuwapatia nyumba za gharama nafuu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, kuna majengo mbalimbali ya Serikali yaliyojengwa kwa ubora kwa kutumia ‘force account’ na kutolea mfano wa baadhi ya majengo hayo ambayo yako katika Mji wa Serikali-Mtumba kuwa ni TARURA na TAMISEMI.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company Dkt. Fred Msemwa amesema wamepokea maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri ya kutumia ‘force account’ na wameshajiandaa kwa ajili ya hilo.

Ameongeza kuwa, walishaanzisha Kampuni ndani ya Watumishi Housing ambayo imetumika kujenga nyumba 61 na nyingine wanatarajia kuzijenga Jijini Dodoma na Mwanza na maeneo mengine nchini.

Ujenzi wa miradi ya nyumba za Watumishi Housing kwa kutumia force account itahusisha njia ya ununuzi wa kazi ya ujenzi kwa kutumia taasisi ya umma au watumishi wake na vifaa au wafanyakazi wa kukodi, njia ambayo itawezesha Watumishi wa Umma kupanga au kununua nyumba kwa gharama nafuu.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company, Dkt. Fred Msemwa wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Watumishi Housing Company ikiwa ni pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoka kukagua moja ya nyumba za Watumishi Housing Company eneo la Gezaulole Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Watumishi Housing Company ikiwa ni pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake.


Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company, Dkt. Fred Msemwa alielezea namna watakavyotekeleza maelekezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ya kutumia ‘force account’ kwenye miradi ya ujenzi wa nyumba za kupangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma kwa bei nafuu wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Ndejembi yenye lengo la kufahamiana na watumishi wa Watumishi Housing Company ikiwa ni pamoja na kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake.

 


Mradi wa nyumba za Watumishi Housing Company eneo la Gezaulole-Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

 

No comments:

Post a Comment