Na.
James K. Mwanamyoto – Chato
Tarehe 19 Disemba, 2020
Wananchi wa Kijiji cha
Nyabilezi na maeneo ya jirani Wilayani Chato watanufaika na huduma za afya
zitakazotolewa katika Kituo cha afya cha Nyabilezi baada Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) kuchangia kiasi cha shilingi milioni 569 kwa lengo la kuboresha
huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Mara baada ya kukagua
maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George
Mkuchika amesema kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na TASAF kitakuwa na
mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya.
Kutokana na umuhimu wa kituo
hicho, Mhe. Mkuchika amewahimiza Viongozi Wilayani Chato kukamilisha ujenzi wa
kituo hicho cha afya ifikapo tarehe 30 Machi, 2021 kama ilivyopangwa ili
wananchi wapate huduma ya afya inayostahili.
Aidha, Mhe. Mkuchika
amewapongeza wananchi wa kijiji cha Nyabilezi kwa kutoa mchango wa fedha na kushiriki
katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa kuchota maji,
kusomba mchanga, kokoto na mawe.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe.
Medard Kalemani ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora kupitia TASAF kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo hicho cha afya
ambacho kikikamilika kitakuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya
katika Kijiji cha Nyabilezi na maeneo jirani.
Pamoja
na pongezi hizo, Mhe. Kalemani amemuomba Mhe, Mkuchika kupitia TASAF kujenga
kituo kingine cha afya katika Kijiji cha Makurugusi ili kupunguza msongamano wa
wananchi watakaofuata huduma za afya katika Kituo cha Nyabilezi.
Awali,
Kituo cha Afya cha Nyabilezi kata ya Bukome kilikuwa ni Zahanati, hivyo
kutokana na umuhimu wa huduma za afya katika kata hiyo, TASAF imetoa kiasi cha
fedha cha shilingi milioni 569 ili kukidhi uhitaji wa huduma za afya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George
Mkuchika akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi na maeneo ya jirani
Wilayani Chato watakaonufaika na huduma za afya zitakazotolewa katika Kituo cha
afya cha Nyabilezi mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho. Kushoto kwake
ni Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani
na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji
cha Nyabilezi na maeneo ya jirani Wilayani Chato wakimsikiliza Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe.
George Mkuchika (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao mara baada ya
kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Nyabilezi Wilayani Chato.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya
Chato, Dkt. Benedicto Ngaiza akisoma taarifa ya ujenzi wa Kituo cha afya cha
Nyabilezi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika alipotembelea kituo hicho ili kukagua
maendeleo ya ujenzi.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa
TASAF, Bw. Paul Kijazi akielezea mchango wa TASAF katika ujenzi unaoendelea
katika kituo cha Nyabilezi Wilayani Chato. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi.
Mbunge wa Jimbo la Chato,
ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani akimshukuru Mhe. Mkuchika
kwa taasisi yake ya TASAF kutoa mchango katika ujenzi wa kituo cha afya cha
Nyabilezi Wilayani Chato. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George
Mkuchika na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Mhandisi Mhe. Robert Gabriel Luhumbi, akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika kuzungumza na wananchi wa Kijiji
cha Nyabilezi na maeneo ya jirani mara baada ya Waziri huyo kukagua maendeleo
ya ujenzi wa Kituo cha afya cha Nyabilezi Wilayani Chato.
No comments:
Post a Comment