Monday, December 14, 2020

MKUCHIKA AWATAKA WATUMISHI WA OFISI YAKE KUANDAA MPANGO MADHUBUTI KUTEKELEZA ILANI YA CCM

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 14 Disemba, 2020

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja taasisi zake wametakiwa kuitekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020-2025 katika eneo la Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili wananchi wanufaike na huduma zitolewazo na ofisi hiyo.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika mara baada ya kupokelewa na Watumishi wa Ofisi yake jijini Dodoma ikiwa ni siku chache tangu ateuliwe na kuapishwa rasmi na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mhe. Mkuchika amesema Ofisi yake na taasisi zote zilizo chini ya Ofisi yake ambazo ni TAKUKURU, MKURABITA, TASAF, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Chuo cha Utumishi wa Umma, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na Wakala ya Ndege za Serikali zinatakiwa zikae na kuandaa mpango madhubuti wa miaka mitano ili kutekeleza ahadi za masuala ya kiutumishi na Utawala Bora zilizoainishwa katika Ilani ya CCM.

“Watumishi wa Umma tunapaswa kuitumikia Serikali iliyoshinda uchaguzi ambayo ni ya CCM na CCM inayo Ilani iliyoiweka Serikali madarakani, hivyo hatuna budi kuitekeleza,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Aidha, Mhe. Mkuchika ametoa rai kwa watumishi kuendelea kutoa ushirikiano katika kipindi hiki alichokabidhiwa tena jukumu la kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuahidi Mhe. Mkuchika na Watumishi ushirikiano katika kuwatumikia Watanzania kama ambayo Mhe. Rais Magufuli anatarajia.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi ameomba ushirikiano kutoka kwa Watumishi na Menejimenti kwa ujumla ili kuhakikisha huduma bora inatolewa kwa wananchi.

Mhe. Mkuchika na Mhe. Ndejembi wamepokelewa leo na Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tayari kwa kuanza kazi rasmi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George akizungumza na watumishi wa ofisi yake mara baada ya kuripoti rasmi. Kushoto kwake ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi. Na kulia kwake ni Katibu Mkuu - UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro. 

Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George mara baada ya kiongozi huyo kuripoti rasmi ofisini kwake jijini Dodoma. 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) mara baada ya kuripoti rasmi na kuanza kazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George akisalimiana na baadhi ya Wakurugenzi wa ofisi yake mara baada ya kuripoti rasmi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Ofisi yake Jijini Dodoma mara baada ya kuripoti rasmi. Kulia kwake ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi na Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro na Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Francis Michael.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika akimkabidhi nyaraka za kiutumishi Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Viongozi hao kuripoti rasmi ofisini na kuanza kazi.












No comments:

Post a Comment